YANGA leo inaanza rasmi mikikimikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheza na African Lyon, ambapo tayari homa ya mpambano huo imepanda kwa watoto hao wa mjini, wakiwahofia zaidi washambuliaji, Donald Ngoma na Amissi Tambwe.

Lyon ambayo katika mchezo wa fungua dimba la michuano hiyo iliibana Azam FC kwa kulazimisha sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, bado inakumbuka uwezo wa Tambwe ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa kinara wa kupachika mabao na vile vile Ngoma ambaye ametokea kuwa straika hatari katika kikosi cha Yanga.

Yanga hawakuanza ligi mwishoni mwa wiki iliyopita kama timu nyingine kutokana na kukabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa wanarejea rasmi wakianza na timu hiyo iliyorejea kucheza Ligi Kuu msimu huu baada ya kushuka daraja 2012/13.

Uwezo wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara unawafanya kuendelea kupewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao sambamba na watani zao wa jadi Simba ambao nao wameonekana kujipanga vizuri.

Licha ya kwamba Kocha Mkuu wa African Lyon, Bernardo Tavares, kusema kuwa watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanawafunga Wanajangwani hao, bado wana hofu na uwezo wa upachikaji mabao wa Ngoma na Tambwe ambao unatajwa kuwepo katika kambi ya timu hiyo.

Kiwewe wanachokipata African Lyon ni kutokana na uwezo waliouonyesha Ngoma na Tambwe msimu uliopita ambapo Tambwe aliweza kuibuka mfungaji bora baada ya kupachika mabao 21.

Yanga watashuka dimbani wakiwa na hasira kubwa baada ya kushindwa kusonga mbele hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na sasa watataka kuona wanaanza vema michuano ya ligi.

Wanajangwani hao wanajua kuwa wapinzani wao wa jadi Simba wamekalia usukani na sasa watataka kufanya kila linalowezekana ili kuwashusha na kupunguza kelele za mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi.

Post a Comment

 
Top