KOCHA Mkuu wa Azam, Zeben Hernandez, ameanza kufungia kazi safu ya ushambuliaji inayoongozwa na John Bocco ili kuwawezesha kufunga mabao katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza na BINGWA juzi,  Hernandez alisema baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliochezwa wiki iliyopita, amebaini upungufu mkubwa katika safu ya ushambuliaji.
Hernandez alisema anafanyia kazi safu ya ushambuliaji ili wafanye vizuri katika mchezo utakaofuata dhidi ya Majimaji utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Alisema moja ya mambo yaliyowakwamisha kutokuondoka na ushindi, ni ubutu wa safu yake ya ushambuliaji kwani licha ya kutengenezewa nafasi na viungo wao walishindwa kuzitumia.
“Mchezo wetu uliopita tulicheza vizuri hasa idara ya kiungo, lakini kulikuwa na upungufu hasa kwenye nafasi ya ushambuliaji na kama wangekuwa makini, nadhani tungeondoka na ushindi, bado sijapata straika wa kiwango cha juu wa kuifanyia ninavyotaka.
Nitajitahidi hawa nilionao niwatengeneze wawe wazuri zaidi, kilichopo naomba nizidi kupewa muda, kwani nikikaa nao vizuri naamini tatizo hili nitalimaliza na tutapata kile ambacho tunakihitaji,” alisema Hernandez.

Post a Comment

 
Top