YANGA wanajua kwamba wanakabiliwa na michuano migumu ya kimataifa na pia wana kazi kubwa ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na sasa wamekaa na kutuliza vichwa vyao kuhakikisha wanalitingisha Bara la Afrika kutokana na usajili watakaoufanya kipindi hiki.

Na kwa kuanzia, wamemleta kocha mpya, George Lwandamina, ambaye atashirikiana kwa ukaribu na Mholanzi Hans van der Pluijm, ambaye amepewa cheo kipya ya Mkurugenzi wa ufundi ambapo wawili hao wanatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa na kujijengea heshima.

Pluijm na Lwandamina wanajua ugumu wa michuano ya kimataifa na sasa taarifa ambazo DIMBA imezinasa zinadai kuwa kuna panga litapitishwa kwa baadhi ya wachezaji ili kupisha silaha mpya zenye makali ya hatari zitakazoweza kupambana na timu zenye majina makubwa barani Afrika.

Kabla ya kupitisha panga hilo, Lwandamina ameomba kuwaangalia kwanza wachezaji wake namna ya uchezaji wao ili kujiridhisha ambapo hayo yote yatafanyika watakapomaliza likizo zao.

Hata hivyo, licha ya Lwandamina kutaka kwanza kuona uchezaji wao, wapo baadhi ambao wanatajwa kwamba panga la kocha huyo halitawaacha salama na tayari majina mapya ya watakaoingia yameshaanza kutajwa.

Majina ambayo yanatajwa kwamba yapo kwenye hatari kubwa ya kupunguzwa ni pamoja na kiraka ambaye anamudu namba zaidi ya moja, Mbuyu Twitte, straika Malimi Busungu, golikipa Ali Mustafa ‘Barthez,’ kiungo Juma Said ‘Makapu,’ beki wa kushoto Oscar Joshua, pamoja na straika Matheo Anthon.

Wengine ni nahodha wa kikosi hicho, Nadir Haroub ‘Cannavaro,’ Obrey Chirwa pamoja na Pato Ngonyani, huku winga, Juma Mahadhi ambaye alisajiliwa kutoka Coastal Union ya jijini Tanga,naye akiwa kwenye mstari mwekundu.

Mbuyu Twitte na Obrey Chirwa wao wanatajwa kutaka kutemwa ili kupisha usajili wa wachezaji kutoka Zesco ya Zambia, Jese Were pamoja na kiungo Meshack Chaila, ambao Lwandamina anawajua vizuri, kwani walimfanyia kazi kubwa alipokuwa nao.

Aidha, Wanajangwani hao wanadaiwa pia kuwa wanataka kuimarisha kikosi chao kwa kuwasajili kiungo mkabaji na Nahodha wa MCC, Kenny Ally, na kiungo mchezeshaji Raphael Daud.

Kwa staili yake mpya maarufu ya ‘mambo kimya kimya,’ inadaiwa Yanga imefikia katika hatua nzuri kwenye mpango wa kuwasajili wawili hao waliopandishwa mwaka 2014 kutoka timu ya vijana ya Mbeya City.

Kuhusu Cannavaro, bado inasemekana wanaumiza vichwa, kwani ni moja ya wachezaji walioitumikia timu hiyo kwa mafanikio makubwa na kwamba heshima yake inaweza kuendelea kumbakisha, japo maamuzi ya mwisho yatatoka kwenye benchi la ufundi.

Post a Comment

 
Top