KOCHA wa Yanga, Mdachi, Hans van Der
Pluijm, ameamua kufunguka kilichopo nyuma ya pazia kuhusiana na shutuma na
malalamiko yanayomwandama beki wa kushoto wa timu hiyo, Haji Mwinyi kuwa
anaporomoka kiwango kila kukicha kwa kuwa hana nidhamu ya kanuni za soka kwa
sasa.
Mwinyi aliyetua Yanga mwanzoni mwa
msimu uliopita akitokea KMKM ya Zanzibar, awali alikuwa kipenzi cha mashabiki
wa timu hiyo kutokana na uwezo aliokuwa akiuonyesha lakini katika mechi za hivi
karibuni, hasa za michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, amekuwa akilalamikiwa
na mashabiki wa Jangwani kuwa kiwango anachoonyesha kimeshuka.
Pluijm amesema kuwa wengi wanashindwa
kuelewa kuwa Mwinyi alitumika muda mrefu na kwamba hivi karibuni amerejea
kutoka kwenye majeraha, hivyo alihitaji muda na sasa ameanza kurejea kwenye
kiwango chake stahiki.
“Hapana, nafikiri kinachozungumzwa
siyo sawa, Mwinyi hajashuka kiwango, ieleweke kwamba kijana ametumika muda
mrefu na baadaye akawa majeruhi lakini kwa sasa ndiyo kwanza anarudi, hata
kwenye mechi ya mwisho ya kirafiki na Mtibwa Sugar alicheza vizuri.
“Bado naendelea kumwangalia katika
mazoezi tunayoendelea kufanya kwa ajili ya MO Bejaia, akiwa fiti zaidi kwa
ajili ya mchezo naweza kumtumia,” alisema Pluijm aliyeiongoza Yanga kutwaa
ubingwa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo sasa.


Post a Comment