SAA chache baada ya kuripotiwa kujiuzulu, imeripotiwa kuwa aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, yuko katika rada za Azam FC ambao inadaiwa kufanya naye mazungumzo ya siri.
Pluijm alimaliza majukumu ya kuinoa Yanga Jumatatu kisha akaandika barua ya kujiuzulu punde tu alipobaini Yanga imefanya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Azam, zinasema kuwa klabu hiyo ya Chamazi imekuwa ikifanya mchakato wa chini kwa chini yakiwemo mazungumzo na uongozi tangu iliporipotiwa kuwa Yanga wako mbioni kumtema.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa Pluijm alilifahamu mapema suala la yeye kutakiwa kuondolewa kwenye benchi la ufundi la Yanga, hivyo akaamua kuzungumza na matajiri hao wa Ligi Kuu Tanzania ambapo walifikia mwafaka.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, hata baada ya Yanga kuwasili nchini mwishoni mwa wiki iliyopita ikitokea Kanda ya Ziwa, wajumbe wawili wa Azam walikwenda uwanja wa ndege na kumchukua kocha huyo kisha wakaenda naye mafichoni kuzungumza naye.
Inasemekana kwamba uamuzi wa Azam kutaka kumchukua Pluijm unatokana na ukweli kwamba klabu hiyo imekuwa haifanyi vizuri tangu kuanza kwa msimu huu ambapo imekuwa chini ya kocha Mhispania, Zeben Hernandez na msaidizi wake.


Hata hivyo, inaelezwa kuwa bado haijajulikana iwapo kocha huyo Mholanzi atachukua nafasi ya kocha mkuu au kuwa mkurugenzi wa ufundi, lakini taarifa nyingine zinadai kwamba katika mipango ya klabu hiyo huenda kocha Mhispania Hernandez na msaidizi wake watahamishiwa katika kituo cha vijana cha klabu hiyo ili kuendeleza na kukuza vipaji kwa vile bado wana mikataba nao.
DIMBA Jumatano lilifanikiwa kuzungumza na Pluijm ambaye alikiri kupata ofa nyingi lakini hakutaka kuweka wazi ni timu gani ambazo zinamhitaji.
Alisema analifahamu vizuri soka la Afrika pamoja na kuwa na uzoefu mkubwa na ana imani hawezi kukosa timu, kwani kuna timu nyingi ndani na nje ya Tanzania zinahitaji huduma yake.
“Nimejifunza vitu vingi nikiwa hapa nchini, pia Yanga wanaweza kuleta mtu wanayemtaka lakini kikubwa ni kwamba mlango mmoja ukifungwa, mwingine hufunguliwa,” alisema Pluijm.
Jana asubuhi, Pluijm huku akiwa amevalia ‘mkanda nje’, alikwenda kuwaaga wachezaji wa Yanga na kuzungumza nao kwa muda kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam na akawatakia kila la heri chini ya kocha mpya ajaye.
Akitoa nasaha zake, Pluijm amewaasa wachezaji kuendelea kujituma na kufanikisha azma yao ya kutetea taji lao kwa mara nyingine, kudumisha nidhamu, kupendana na kutanguliza mbele masilahi ya timu kuliko masilahi binafsi.
Pluijm pia aliagana na wasaidizi wake Juma Mwambusi, anayeiongoza timu kwa sasa, kocha wa makipa, Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, mtunza vifaa vya timu, Mahmoud Omar ‘Mpogoro’ na daktari wa timu, Edward Bavu.

Post a Comment

 
Top