SAADA SALIM NA ELIZABETH JOSEPH (RCT)
BAADA ya kuonyesha kandanda la kuvutia na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwishoni mwa wiki iliyopita, Wekundu wa Msimbazi, Simba wameapa kuwashushia kipigo JKT Ruvu leo na kuzidi kujichimbia kileleni.
Jeuri hiyo ya Simba inatokana na uwezo mkubwa wa safu yao ya ushambuliaji inayoundwa na Laudit Mavugo, Fredrick Blagnon pamoja na Ibrahim Ajib ambao wamekuwa chachu ya ushindi katika klabu hiyo.
Simba wanashuka Uwanja wa Uhuru leo wakiwa wageni wa JKT Ruvu na wanajua kwamba wapinzani wao Yanga, wataianza ligi kesho dhidi ya African Lyon hivyo ili kuwakimbia lazima washinde kwa idadi kubwa ya mabao.
Katika mazoezi ya Wekundu hao wa Msimbazi ambayo yamekuwa yakifanyika Uwanja wa Boko Veterani, kocha mkuu wa kikosi hicho, Joseph Omog, amekuwa akiwafua vikali washambuliaji wake hao lengo kubwa likiwa kufunga mabao mengi iwezekanavyo.
Washambuliaji hao walionekana kumwelewa vizuri kocha wao huyo kutokana na jinsi walivyokuwa wakifunga mabao ya maana na kuwafanya mashabiki waliokuwa wakihudhuria mazoezi hayo kushangilia kila mara.
Mavugo na Blagnon wamekuwa kivutio kikubwa kutokana na uwezo wao wa kucheka na nyavu ambapo katika mchezo uliopita dhidi ya Ndanda kila mmoja alifunga bao huku lingine likiwekwa wavuni na Shiza Kichuya ambapo leo wanatarajiwa kuzidi kuuwasha moto.
Jambo la kufurahisha kwa Wanasimba ni kwamba, wachezaji wao wote muhimu wapo fiti kuwavaa maafande hao na kocha mkuu wa kikosi hicho, Omog, amesema hakuna kulala na badala yake ni mwendo wa ushindi mwanzo mwisho.
Omog aliliambia BINGWA kuwa malengo yake ni kuhakikisha kikosi hicho kinashinda michezo yake yote ukiwamo wa leo ili kutwaa ubingwa ikizingatiwa kuwa Wekundu hao wa Msimbazi wana misimu minne mfululizo bila kufanya hivyo.
“Nilivyokuja niliwaahidi mashabiki kwamba tutafanya kitu tofauti, naamini ndiko huko tunakoelekea kwani kile ambacho ninawaelekeza wachezaji wangu ndicho wanachokifanya, nadhani malengo yetu ya kushinda kila mchezo yatatimia,” alisema.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Malale Hamsini, alisema haogopi chochote na badala yake wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na lengo moja tu la kusaka pointi tatu kwani walifanya hivyo msimu uliopita.
Msimu uliopita mchezo wa funga dimba Simba walilala kwa mabao 2-1 mbele ya maafande hao ambao ilikuwa ni lazima kushinda ili kuepuka mkasi wa kushuka daraja na sasa wametamba kuendeleza ubabe huo.
Kama Simba watashinda mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao watazidi kujichimbia kileleni mwa msimamo na kuwaacha wapinzani wao wa jadi, Yanga ambao wataianza ligi kesho dhidi ya African Lyon.

Post a Comment

 
Top