SIMBA imebadilisha staili ya mauaji kwa kila timu itakayokutana nayo katika mechi zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya Kocha Mkuu, Joseph Omog, kupata dawa na timu ‘zinazopaki basi’.
Simba kwa hivi sasa inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Polisi, Kurasini wilayani Temeke, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Omog alisema atalazimika kubadili staili ya uchezaji kwa kucheza kwa malengo huku wakitafuta njia za kufunga mabao katika wakati mgumu kama ilivyokuwa kwenye mchezo wao na JKT Ruvu.
“Tulicheza vizuri lakini hatukupata ushindi si matokeo mabaya, lakini pia si mazuri kwa sababu ligi ina ushindani unapopata matokeo tofauti na ushindi inakuwa mbaya na sasa nimeona tubadili mfumo wa uchezaji wetu tuache kupiga pasi nyingi na sasa tunatakiwa kwenda mbele kutafuta ushindi na kila mchezaji wangu nataka aongeze umakini awapo uwanjani,” alisema Omog.



Kocha huyo alisema pamoja na kwamba matokeo ya suluhu si mabaya, lakini kama kocha hayajamfurahisha na ndiyo maana amepanga kubadili mfumo wa uchezaji kwa kutaka wacheze kwa kasi hasa wanapovuka mstari wa kati na pia atawabadili baadhi ya wachezaji ambao watashindwa kuendana na mfumo huo.
Kocha huyo alisema baada ya kuona mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huo, amefanyia kazi kwa kuhakikisha anakuwa makini kwa kila idara katika timu yake.
“Nimeona mechi yetu iliyopita kwani JKT Ruvu walikuwa wakizuia zaidi, hivyo naendelea na programu yangu ya kuanza kuwanoa washambuliaji nikichanganya na viungo baadaye nikimalizia na mabeki,” alisema.
Omog alisema anatumia vyema siku chache za mapumziko kuendelea na programu yake ili kuhakikisha wanafanya vyema katika michezo iliyobakia waweze kupata ushindi kwa kila mechi.
Alisema anaamini timu zote watakazokutana nazo zitawakamia hivyo watahitaji kushambulia kwa nguvu huku wakizuia.
CHANZO: Dimba

Post a Comment

 
Top