HABARI ni kuwa kuna uwezekano mkubwa
wa Yanga kutomtumia beki wake, Hassan Kessy kutokana na kesi yake kuonekana
kuwa kizungumkuti huku ikionekana kuwaendea vibaya wahusika hao.
Kessy alisajiliwa Yanga hivi karibuni
na jina lake likapelekwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika orodha ya
waliosajiliwa kwa msimu wa 2016/17, lakini kitendo cha Simba kugoma kutoa barua
ya kumuacha, kinamaanisha kuwa hataweza kuichezea Yanga ikiwa suala hilo
halitapatiwa ufumbuzi.
Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit,
amekiri kuwa mpaka kufikia jana walikuwa hawana mamlaka ya kumtumia beki huyo kwa
kuwa hawajapata barua ya Kessy kuachwa na Simba wanaotaka walipwe kwa kile
walichodai alisajiliwa wakati akiwa na mkataba na Simba.
Taarifa za ndani kutoka TFF zimesema ishu
hiyo ni ngumu TFF kuiingilia badala yake ni busara za Simba kuketi na mchezaji
mwenyewe kulimaliza, lakini vinginevyo Yanga inaweza kuingia ‘chaka’ na akawa
anaishia kufanya mazoezi tu.
“Inaonekana Yanga wanataka kuiruka
kesi yenyewe, wameshaona walifanya kosa kumsajili kabla ya mkataba wake kuisha
pale Simba, sasa Simba waliwataka fidia ya dola 60,000 (zaidi ya Sh milioni 120)
ili watoe barua hiyo lakini Yanga hawataki.
“Wanaogopa kuzilipa maana wakithubutu
tu, itazaa kesi nyingine ya kumsajili mchezaji wakati ana mkataba na timu
nyingine, ndiyo maana nao wako kimya. Yote kwa yote, Kessy bila barua kutoka
Simba, hawezi kuichezea Yanga popote pale,” alieleza mtoa taarifa.
Moja ya ushahidi wa Simba ni baada ya
kumuona beki huyo akiwa na jezi ya Yanga, Mei 25, 2016 katika mchezo wa Kombe
la FA kati ya Yanga na Azam FC huku mkataba wake na Simba ukiwa hai kwani
ulikuwa unamalizika Juni 15, 2016.


Post a Comment