KAMA mchezaji umebahatika
kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Mcameroon, Joseph Omog ndani ya Simba basi
unatakiwa kupambana kwani ukizingua tu, benchi litakuhusu.
Hiyo ni kauli ya Kocha
Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, aliyoitoa mara baada ya mchezo wa
kirafiki na AFC Leopards ambapo Simba ilishinda kwa mabao 4-0.
Lakini wakati msaidizi akisema hivyo,
bosi wake, Joseph Omog amewapa masharti magumu wachezaji wa kimataifa akiwemo
Mrundi Laudit Mavugo kwa kuwambia ole wake atakayekaa benchi.
Omog amesema kuwa hakuna mchezaji wa
kimataifa ambaye atakaa benchi kutokana na kuonyesha uwezo mdogo, badala yake
kila mmoja anatakiwa ajitume ili aweze kupata nafasi ya kucheza katika kikosi
cha kwanza.
“Usajili nilioufanya unaendana na
uhitaji wa kikosi changu na nimesajili wachezaji wa kimataifa kwa kuangalia
kila mmoja anakuwa na kiwango na kila mmoja nahitaji acheze labda itokee mtu
awe anaumwa kwani mchezaji wa kimataifa anatakiwa awe na uwezo zaidi ya wazawa.
“Kwa sasa bado sijapata kikosi cha
kwanza japokuwa kuna baadhi ya wachezaji wanaonyesha kuwa na kiwango kizuri cha
kucheza katika kikosi cha kwanza. ambaye atakaa benchi kutokana na kuonyesha
uwezo wa chini huyo atakuwa hatufai,” alisema Omog.
Wachezaji wa kimataifa waliopo Simba
ni Vicent Angban, Mavugo, Juuko Murshid, Musa Ndusha, Janvier Bokungu, Fredrick
Blagnon na Method Mwanjali.
Upande wa Mayanja alisema
usajili wao walioufanya chini ya Omog umekidhi viwango walivyokuwa wanavihitaji
kwa ajili ya kuleta ushindani wa namba.
Mayanja amesema msimu
uliopita hawakuwa na kikosi bora kwa ajili ya ushindani, hasa kwa wachezaji
waliokuwa wakianza kikosi cha kwanza na wale waliokuwa benchi lakini sasa
wanajivunia ushindani mkali ambao wanaamini utawasaidia kufanya vizuri.
“Yapo matarajio makubwa
kwa mashabiki wa Simba kuuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu ujao, kujiamini huko
kunatokana na uwezo wa mchezaji mmojammoja ambao upo juu.
“Hivi ndivyo timu
inavyotakiwa kuwa, lazima wawepo wachezaji watakaoleta ushindani, wale
wanaokuwa benchi na wanaokuwa uwanjani wanacheza, wote uwezo wao unatakiwa kuwa
sawa, kukosa hali hiyo kulichangia kutunyima ubingwa msimu uliopita,” alisema
Mayanja.
CHANZO: CHAMPIONI IJUMAA


Post a Comment