BEKI wa kati wa Yanga, Mtogo, Vincent
Bossou, ameweka wazi kuwa kutokana na kiwango cha hali ya juu kilichoonyeshwa
na Simba, ni wazi kuwa wana kazi kubwa watakapokutana nao kwenye kuwania
ubingwa.
Bossou ameyasema hayo kutokana na
kuishuhudia Simba ikicheza dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, Jumatatu ya wiki hii
ambapo Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo
uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Bossou alisema kuwa timu hiyo
imebadilika mno ukilinganisha na msimu uliopita ambapo hayo yametokana na
kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa ambao wanaweza kuwapa presha katika
kuwania ubingwa kwa msimu huu.
“Simba hii imebadilika sana kwa jinsi
nilivyoiona leo (Jumatatu hii) na kiukweli nikiri kwamba sasa wana wachezaji
ambao wanaweza kutupa presha tutakapokutana nao lakini hata kwenye mbio za
kuwania ubingwa kwa msimu huu.
“Lakini tayari tumeshawaona na hata
Kocha Hans van Der Pluijm naye amewashuhudia, hivyo tutakachoenda kukifanya ni
kuandaa mbinu na namna ambayo tutaweza kuwadhibiti pale tutakapokutana nao,” alisema
Bossou raia wa Togo ambaye alikuwepo Uwanja wa Taifa kuishuhudia Simba.
Kuhusu mshambuliaji wa Simba, Laudit
Mavugo, Bossou alisema: “Ni mchezaji mzuri lakini huu ni mchezo wa kirafiki
inawezekana Wakenya labda hawakuwa vizuri.”
Simba imeshindwa kufanya vizuri kwa
misimu minne mfululizo hali ambayo ilizipa nafasi Yanga na Azam FC kutamba
Yanga wakienda mbele zaidi kwa kujiita Wakimataifa kutokana na ushiriki wao
kwenye michuano ya kimataifa huku Simba wakishindwa kufuzu kutokana na kuonyesha
kiwango cha chini.
Usajili wa wachezaji wa kimataifa
waliopo Simba kina Vicent Angban, Mavugo, Juuko Murshid, Musa Ndusha, Janvier
Bokungu, Fredrick Blagnon na Method Mwanjali umewapa imani Wanasimba kuamini
kuwa huu ni mwaka wao wa kufanya vizuri.
CHANZO: CHAMPIONI IJUMAA
Post a Comment