FOWADI
mpya wa Simba aliye kwa mkopo, Ame Ally ‘Zungu’ amekiangalia kikosi cha timu
hiyo na kutamka kuwa kwa jinsi mambo yalivyo, hana namna zaidi ya kujipanga
kisawasawa kama kweli anataka kuonekana kutokana na kasi ya ajabu iliyoonyeshwa
na mafowadi, Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi.
Zungu,
ametua Msimbazi akitokea Azam kwa mkopo, hata hivyo picha inayojionyesha hana
nafasi kikosi cha kwanza mbele ya wakali hao ambao Jumatatu wiki hii
waliwakosha mashabiki kwa kuhusika katika mabao yote manne wakati Simba
ikiichapa AFC Leopards ya Kenya mabao 4-0 katika mchezo wa Tamasha la Simba
Day.
Katika mchezo huo, Ajib alifunga mabao mawili
huku Mavugo akifunga moja na kutengeneza jingine kwa Shiza Kichuya lakini
kilichowachanganya mashabiki ni jinsi walivyoweza kuelewana vizuri katika kutengeneza
mabao hayo kana kwamba wamezoeana siku nyingi.
Katika
mahojiano na gazeti hili, Zungu alikiri kikosi kicho kujaa ushindani kila safu,
hali inayomlazimu kujitutumua mazoezini ili kumshawishi kocha.
“Kiukweli kuna ushindani mkubwa, kila mmoja
anaonekana ana ari ya ushindani na wengi wanajua, hivyo haina jinsi lazima ni
kupambana kwelikweli na amini pia nafasi inaweza kupatikana japo ushindani si
wa kitoto,” alisema fowadi huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.


Post a Comment