MKUU wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, ametamka kuwa jana Ijumaa
ndiyo alianza kazi rasmi kwenye timu hiyo.
Kauli hiyo, ameitoa ikiwa ni siku chache tangu
mwenyekiti wa timu hiyo, Yusuf Manji kuagiza Muro aanze kazi mara baada ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kumfungia mwaka mmoja.
TFF ilimfungia Muro hivi karibuni kufuatia
madai ya kulishambulia shirikisho hilo, hivyo atatakiwa kukaa kwa kipindi
hicho.
Muro alisema ameanza kazi rasmi baada ya
kumaliza likizo yake Agosti 2, mwaka huu na jana aliripoti ofisini kwa mara ya
kwanza.
Muro alisema, taarifa za kufungiwa amezisikia
lakini hana nakala ya barua ya hukumu yake, hivyo ameiomba TFF kumpelekea barua
hiyo kwa ajili ya kuipitia na kujua sababu iliyowafanya wamfungie.
Aliongeza kuwa, mara baada ya kupokea nakala
hiyo, haraka atakutana na viongozi wake kwa ajili ya kupitia kanuni na sheria
zilizotumika yeye kufungiwa mwaka mmoja.
“Naomba nichukue nafasi hii kuwatangazia
Wanayanga kuwa, mimi leo (jana) ndiyo nimeanza kazi rasmi Yanga na niliripoti
kazini tangu Agosti 2, mwaka huu.
“Nimefika hapa ofisini na kupata taarifa za
mimi kufungiwa, sikatai kufungiwa lakini kikubwa ninachoomba ni kupatiwa nakala
ya barua ya hukumu kutoka TFF na badala ya hapo ndiyo mengine yafuate.
“Mara baada ya kupata nakala hiyo, kikubwa
ninataka kujua sababu ya mimi kufungiwa ili nijue kanuni na sheria iliyotumika,
baada ya hapo nijue nikate rufaa kwa kosa lipi, lakini siyo kama hivi
wanavyofanya TFF,” alisema Muro.


Post a Comment