KIUNGO wa Azam FC, Himid Mao, jana aliingia katika
matatizo baada ya kudaiwa kumkwida na kumpiga ngumi askari wa usalama
barabarani maeneo ya Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Spotiripota ilipowasiliana na Kamanda wa
Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema amepata taarifa hizo
pia.
“Ni kweli na mchezaji huyo anashikiliwa kwenye
kituo cha Stakishari, lakini vizuri uzungumze na RPC wa Ilala kwa kuwa suala
hilo linakwenda kwenye jinai,” alisema Kamanda Mpinga.
Akizungumzia tukio hilo ambalo inadaiwa
lilitokea jana asubuhi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alikiri
kutokea kwa tukio hilo ambapo alifafanua chanzo ni mwendo kasi wa gari ambayo
alikuwa akiendesha mchezaji huyo.
“Ni kweli kabisa tukio hilo limetokea asubuhi
ya leo (jana), huyo mchezaji wa Azam inadaiwa alikuwa katika mwendo kasi ndipo
askari alipomsimamisha lakini wakati mazungumzo kati yao yakiendelea,
inaonekana walipishana kauli na ndipo mchezaji huyo alipomkwida shati lake na
kumtwanga ngumi ya usoni.
“Inasemekana amemjeruhi vibaya usoni na hivi
sasa mchezaji huyo anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Sitakishari kwa ajili
ya mahojiano zaidi ila taarifa za kina juu ya suala hilo bado hazijanifikia
ambapo kwa sasa nasubiri ripoti ya maandishi ili niweze kujua eneo sahihi
lilipotokea tukio hilo, jina la mtuhumiwa ambaye ni mchezaji wa Azam pamoja na
askari aliyepigwa,” alisema Hamduni.
Alipoulizwa Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar
Idd juu ya tukio hilo alisema: “Kuna tukio limetokea kuhusu Himid, maofisa wetu
wanafuatilia, watakaponipa taarifa nitakuwa na muda mzuri wa kulielezea lakini
siyo kwa sasa.”



Post a Comment