TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imefunguka rasmi sababu
za kumshikilia na kumweka ndani Rais wa Simba, Evans Aveva.
Aveva alishikiliwa tangu juzi Jumatano na kulala ndani
kwenye Kituo cha Polisi cha Urafiki jijini Dar kabla ya kutolewa kwa dhamana
Alhamisi huku chanzo cha yote kikiwa ni baada ya Takukuru kubaini alifanya
uchepushaji wa fedha za mauzo ya fowadi, Emmanuel Okwi walizolipwa Simba na
Etoile du Sahel dola laki tatu ambazo zilitolewa kwenye akaunti ya klabu na
kuhamishiwa kwenye akaunti yake kabla ya kuanza kusambazwa huku nyingine
zikihamishiwa katika akaunti moja ya nchini Hong Kong.
Msemaji wa Takukuru, Tunu Mlei amesema, kutokana na
mazingira hayo, walihisi uwepo wa rushwa hivyo kuanza kuchunguza.
Tunu amefunguka huku akisisitiza kuwa iwapo atabainika
na makosa katika sheria ya uchepushwaji, anaweza kufunguliwa mashtaka
mahakamani.
“Kwa sasa bado tunaendelea na uchunguzi na kwa mujibu wa
sheria zetu haziniruhusu kusema nini kinaendelea kwenye uchunguzi,” alisema.
“Muda wa kuwachunguza itategemea. Kuna process
(mchakato) zake. Kwa sasa tupo katika sheria No.11 kifungu cha 29 ya mwaka 2007
inayohusu uchepushwaji wa fedha, tukimaliza uchunguzi kazi yetu ni kupeleka
faili kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini, ndiye mwenye kuamua kesi iende
mahakamani ama la.”
Akafunguka zaidi kuwa kwa sasa wanafanya kazi na
Serikali ya Hong Kong.
“Kama unavyojua uchunguzi unahusishwa na nje ya nchi kwa
kuwa kuna hela zimekwenda Hong Kong, hivyo tunashirikiana na serikali ya huko
kujua zilikwenda kufanya kitu gani,” aliongeza.
Tunu amesema iwapo uchunguzi utabaini kuna mazingira ya
rushwa, sheria itachukua mkondo wake lakini sheria ya uchepushaji wa hela pia
ina adhabu yake.
“Kama nilivyosema tupo kwenye sheria ya uchepushaji,
ambayo pia ina adhabu yake lakini siwezi kuisema maana vifungu vinaweza
kuongezeka kulingana na uchunguzi utakavyofungua mambo mengine,” alisema Tunu.
Licha ya mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage
kusisitiza Etoile du Sahel kuilipa Simba fedha hizo muda mrefu, viongozi chini
ya Aveva wamekuwa wakiruka kimanga wakisema bado hela hiyo haijaingia kwenye
akaunti zao.
Simba ilimuuza Okwi mwaka 2013 wakati wa utawala wa
Mwenyekiti Ismail Aden Rage, hata hivyo hakukaa sana kabla ya kwenda SC Villa
ya Uganda, kisha Yanga kabla ya kurejea Simba ambako alikaa msimu mmoja kabla
ya kuuzwa kwa dola 110,000 kwenda SonderjyskE ya nchini Denmark, mwaka juzi.

Post a Comment