MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji, ameibuka upya baada
ya juzi kutangaza kutaka kuikodi klabu hiyo kwa muda wa miaka kumi ili kuifanya
kuja kuwa moja ya klabu kubwa ndani na nje ya nchi.
Juzi Jumamosi Yanga ilifanya Mkutano Mkuu wa Dharura kwa
wanachama wa klabu hiyo ambapo Manji alitangaza ombi lake hilo ambalo sasa kazi
imebaki kwa Baraza la Wadhamini la Klabu ya Yanga kukubali au la.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili jijini
Dar, Manji alisema amepanga kufanya mambo makubwa ndani ya klabu hiyo endapo tu
ombi lake hilo litakubalika, huku akiwashangaa wanachama wa klabu hiyo kwa
kushindwa kumuuliza maswali katika mkutano huo.
Wanachama
wasimuogope
“Unajua nilikuwa nashangaa sana kuona kila
ninachokiongea hakuna hata mwanachama aliyepinga wala kuuliza swali ambalo
ningeliona kweli hawa watu wanahitaji ufafanuzi.
“Wao kila nikiongea wanaitikia ndiyo, nilishangaa
sana, yaani hawajauliza kwa nini nimeamua kutangaza kuikodi kwa muda wa miaka
kumi na siyo mitano au 20, kutokana na hilo, ndiyo maana leo (jana) nimeamua
kuwaita ninyi wanahabari kwenda kuwapa ufafanuzi wa mkutano ule.
“Siwezi kutoa ahadi moja kwa moja kwamba ndani ya
miaka hiyo kumi nitafanya nini kwa Yanga kwa sababu naogopa inaweza isiwe hivyo
nikaja kuonekana muongo, lakini nitaumia sana kuona sijafanikiwa halafu MO
amefanikiwa na Simba yake.”
Kubadili mfumo
wa uendeshaji
“Yanga kwa kipindi kirefu nilichokuwa ndani ilikuwa
ikiendeshwa kwa mfumo wa hasara, tazama mwaka jana tulipata hasara ya zaidi ya
bilioni 1.5 na mwaka huu tunaelekea kupata hasara ya bilioni 1.9, sasa nikija
kuikodi kwa miaka hiyo kumi, hasara hizi hazitakuwa kwenye klabu bali zitakuwa
zangu.
“Lakini kwa kuwa tayari nimetangaza faida
itakayopatikana asilimia 75 zitakuwa zangu na 25 zinaenda kwa klabu, basi mambo
yakienda kama nilivyopanga Yanga itakuja kuwa moja ya klabu kubwa hapa nyumbani
na nje ya hapa.
“Tutakuwa na uwanja wetu, usafiri bora kama ndege,
kuwa na benki yetu na vingine vingi ambavyo ni mahitaji muhimu kwa klabu.”


Post a Comment