KUFUATIA lile sakata la Rais wa Simba, Evans Aveva wiki iliyopita kukamatwa na kuhojiwa kabla ya kuachiwa kwa dhamana, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imemtaka kuripoti katika makao makuu yao kesho Jumanne ili kuendelea kuhojiwa.
Aveva alikumbwa na majanga hayo na kulala ndani kwenye Kituo cha Polisi cha Urafiki kilichopo jijini Dar, baada ya kubainika alifanya uchepushaji wa fedha za mauzo ya aliyekuwa straika wa timu hiyo, Emmanuel Okwi walizolipwa baada ya kumuuza kwenye timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Fedha hizo ambazo ni dola laki tatu, inadaiwa zilitolewa kwenye akaunti ya Klabu ya Simba na kuhamishiwa kwenye akaunti yake binafsi kabla ya kupelekwa kwenye akaunti nyingine iliyopo nchini Hong Kong.
Kutokana na hali hiyo, Takukuru ikahisi kuna kila dalili za kuwepo kwa mazingira ya rushwa hivyo kuamua kulifuatilia suala hilo ambapo lilianza kwa kumtia mikononi Aveva, kabla ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba nao kuitwa kwa ajili ya mahojiano.
Chanzo cha habari kilichoomba hifadhi ya jina lake, kilisema: “Ameambiwa Jumanne ndiyo aende kujieleza tena kwenye makao makuu ya Takukuru, hivyo kutokana na hilo kesho (leo) Jumatatu tutakuwa naye kwenye tamasha letu la Simba Day.”

Alipopigiwa simu rais huyo, muda wote simu yake ilikuwa haipokelewi, licha ya juhudi za mara kwa mara kumtafuta.

Post a Comment

 
Top