July 7, 2025 03:51:53 AM Menu






LAUDIT Mavugo asicheze Simba? Haiwezekani, kwa sababu tayari uongozi wa miamba hiyo ya Msimbazi umejipanga kupambana kuhakikisha straika huyo Mrundi anakuwa sehemu ya kikosi cha Joseph Omog kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Kumekuwa na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikidai kuwa Mavugo hawezi kucheza Simba msimu ujao kwa sababu bado ana mkataba na klabu yake ya Vital’O ya Burundi, lakini uongozi wa Simba umefunguka na kudai kuwa iwe isiwe lazima staa huyo avae jezi zao msimu ujao.

Akizungumza na BINGWA jana Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele, alisema kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na Vital’O kwa ajili ya kukamilisha usajili wa straika huyo ambaye tayari amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi.

Kahemele alisema tayari hatua ya kwanza katika usajili wa staa huyo imeshakamilika kwa makubaliano ya pande mbili kati ya klabu na mchezaji na kinachosubiriwa sasa ni hatua ya pili ya makubaliano ya klabu na baadaye kutumiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa  (ITC).

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema hata kama Vital’O wakigoma kutuma ITC kwa muda mwafaka watapiga hodi kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ili kupata kibali cha kumchezesha Mavugo.

“Kuna kipengele Fifa ambacho kinaruhusu mtu kupewa kibali cha muda ndani ya siku 14 kama klabu yake ikigoma kutuma ITC, hivyo kama Vital’O wakigoma basi tutaenda hatua inayofuata kuhakikisha Mavugo anacheza Msimbazi msimu ujao,” alisema.

Akizungumzia sakata hilo la usajili kwa upande wake Rais wa klabu ya Vital’O, Bikolimana Benjamin, ametoa kauli ambazo zinaweza kuishangaza Yanga ambayo kipindi fulani iliwahi kutajwa kumfukuzia kimya kimya Mavugo baada ya kudai kuwa timu yake iko tayari hata kuwaazima Simba straika huyo.

“Sisi na Simba hatuna tatizo lolote hivyo hata kama wakishindwa kutoa fedha tunaweza kuwaazima mchezaji wakamtumia kwa mwaka mmoja na baadaye akarudi Vital’O.

“Siwezi kutaja fedha yoyote ile viongozi wa Simba wanajua nini kinaendelea na kuhusu mkataba ni kweli kuwa bado Mavugo ana mkataba na sisi ila siwezi kusema unamalizika, lakini Simba wanajua,” alisema.
11 Aug 2016

Post a Comment

Emoticon
:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top