KOCHA wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm,
ameshindwa kujizuia na kuanza kuwamwagia sifa wachezaji wake waliotua klabuni
hapo hivi karibuni; Mzambia, Obrey Chirwa na Andrew Vincent ‘Dante’ akidai kuwa
ni chaguo sahihi kuelekea kwenye msimu ujao unaotarajiwa kuwa mgumu zaidi.
Pluijm ambaye si mwepesi wa kuzungumzia mchezaji
mmojammoja, alilazimika kuwazungumzia wachezaji hao kutokana na uwezo wa juu
waliouonyesha katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar juzi Jumamosi na kumalizika kwa suluhu.
Kuhusu Dante, Pluijm alisema si mchezaji wa kukaa
benchi na kwa uwezo anaouonyesha hajajua itakuwaje kuelekea msimu ujao,
kutokana na ushindani ulioongezeka katika nafasi ya beki wa kati tangu alipotua
katika kikosi hicho akitokea Mtibwa.
“Umemuona alivyokuwa anacheza leo (juzi), mipira
yote ya juu alikuwa anaimudu, pasi zake zote alizopiga zilifika sehemu husika,
kasoro moja tu. Amedhihirisha si mchezaji wa kuja kukaa benchi, maana kiwango
chake kinashabihiana na mabeki wengine aliowakuta hapa (Kelvin Yondani, Vincent
Bossou na Nadir Haroub ‘Cannavaro’). Tusubiri kuona msimu ukianza itakuwaje,
maana ni mchezaji mwenye kiwango cha juu.
“Umeona hata Chirwa amecheza vizuri sana, amekuwa
akipambana kila mechi, mfano leo alikuwa akitengeneza nafasi nyingi, amejaribu
kupenya kufunga kila wakati lakini alikosa msaada kidogo tu, ni dalili nzuri
kuelekea msimu ujao,” alisema Pluijm.
Dante, Chirwa ni kati ya wachezaji waliosajiliwa
Yanga hivi karibuni kwa ajili ya kuiongezea nguvu timu hiyo katika michuano ya
Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na ligi kuu msimu ujao. Wengine ni kipa Beno
Kakolanya aliyetokea Prisons, Hassan Kessy (Simba) na Juma Mahadhi (Coastal
Union).
Post a Comment