WAKATI Barcelona ikitarajiwa kuivaa Liverpool, leo Jumamosi,
straika wa Barcelona, Luis Suarez amesema anafurahia kuona anakutana na rafiki
zake aliocheza nao muda mrefu.
Timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa Wembley ikiwa ni
michuano ya International Champions Cup ambayo ni mwendelezo wa mechi za
kujiandaa na msimu mpya, hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Suarez kukutana dhidi
ya timu yake hiyo ya zamani tangu alipoondoka mwaka 2014.
Kwa sasa Suarez ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha
Barcelona, heshima aliyoitengeneza akiwa Liverpool ya kufunga mabao 82 katika
mechi 133 ilimfanya kuwa kipenzi cha wengi kikosini hapo mpaka sasa.
"Ni wakati mzuri kwa mashabiki. Nina marafiki wengi pale,
nafikiri ni jambo zuri kukutana nao na kucheza dhidi yao,” alisema Suarez na
kuendelea:
"Kwa mchezaji unapocheza mbele ya mashabiki 90,000 ni
ndoto kuwa kweli. Mashabiki wa Liverpool ni watu wa kipekee duniani na
ninadhani wana hamu na mchezo huo pia.”
“Kila mtu anajua jinsi Liverpool ilivyo muhimu katika maisha
yangu binafsi na ya soka. Mtoto wangu wa pili nilimpata nikiwa hapo na
ninakumbuka kuwa na nyakati nzuri sana hapo.”


Post a Comment