WAKATI kukiwa na taarifa kuwa mshambuliaji wa Simba, Ibrahimu Ajib, ametimkia nchini Misri kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa, wakala wa zamani wa mchezaji huyo, Juma Ndambile, ameibuka na kusema mchezaji huyo kamwe hawezi kufanikiwa kutokana na tabia zake.
Itakumbukwa kuwa mapema mwaka huu Ndambile alimfanyia mipango Ajib ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Lamontville Golden Arrows FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Afrika Kusini, lakini mshambuliaji huyo alishindwa kujiunga nayo kutokana na kuwa na mkataba na klabu yake ya Simba.
Akizungumza na BINGWA kutoka nchini Marekani, Ndambile alisema amesikia kupitia vyombo vya habari kuwa mchezaji huyo amekwenda nchini Misri kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa na kusema kamwe hawezi kufanikiwa kutokana na tabia zake za utoto alizonazo Ajib.
“Nimesikia kuwa katoweka Simba. Labda nikwambie kitu tu, huyo hawezi kucheza mpira wa kulipwa sehemu yoyote duniani. Anawatingisha tu Simba lakini hana jipya,” alisema Ndambile.
Ndambile alisema viongozi wa Simba wasitarajie faida yoyote kutoka kwa mshambuliaji huyo kwani tabia zake za majivuno pamoja na kujiona ni supastaa ndizo zinazomfanya ashindwe kupiga hatua mbele.
“Mimi nimekaa naye kwa muda mfupi nchini Afrika Kusini, lakini niliomba siku ziishe turudi Bongo kutokana na mambo ya ajabu kabisa aliyokuwa akiyafanya halafu unasema kuna mchezaji hapo,” alisisitiza Ndambile.
Aliongeza kuwa kutokana na tabia zake ni ngumu kupata timu katika ukanda huu wa Afrika, barani Ulaya au popote pale duniani, mpaka hapo atakapoweza kujitambua na kujielewa.
“Ukiwa mchezaji kuna vitu vingi sana unatakiwa kuwa na upeo navyo na si vinginevyo, kitu ambacho kinawashinda wanasoka wengi wa Tanzania. Ndiyo maana kila kukicha watabakia kuwa hapa hapa,” aliongeza Ndambile.
Alisema Ajib ataendelea kuitesa Simba na wala si timu nyingine na hiyo ni kutokana na ukweli kwamba Wekundu hao wa Msimbazi wamempa nafasi ya kujiona supastaa ndani ya kikosi cha timu hiyo.
“Ajib ni wa Simba tu. Hawezi kucheza kokote kule hata Yanga hawatamweza kutokana na tabia zake, watamfukuza ndani ya muda mfupi,” alisisitiza.
Alisema kitendo cha viongozi wa Yanga kuwa katika mipango ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo, pia kimemfanya kumwongezea kiburi na kumfanya ajione bonge la staa.
Ajib hivi sasa ni miongoni mwa washambuliaji nyota waliopo katika kikosi cha Simba na ametokea kuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi.
Post a Comment