UKIMWAGA ugali wenzio wanamwaga unga,
sasa Simba imepanga kumkomesha nahodha wake, Jonas Mkude, kwani akiendelea
kudengua kusaini mkataba mpya wao watamsajili kiungo mwenye uwezo zaidi yake.
Achana na hiyo, Simba pia imepanga
kumpiga benchi Mkude katika michezo yao inayokuja ya mzunguko wa pili wa Ligi
Kuu Bara, kwani haijapendezwa na kitendo cha nahodha huyo kusema yupo tayari
kusaini hata Yanga kama atazinguliwa na timu yake hiyo.
Tayari Mkude amevuka mtego wa kwanza
aliowekewa na Simba kwamba kama asingetokea mazoezini angekatwa mshahara wake
lakini kiungo huyo ameenda mara moja katika mazoezi hayo huku wenzake wakifanya
mara tatu. Jana ilikuwa siku ya nne ya mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi
Kurasini jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili
ya Simba, ameliambia Championi Jumamosi: “Tunataka kumsajili kiungo mkabaji
mwingine katika usajili huu, haya mambo ya Mkude hayajatupendeza.”
“Inaonekana Mkude anatudengulia kuongeza
mkataba mwingine wa miaka miwili kutoka ule wa sasa ambao unaisha Januari
mwakani, awali tulipanga kuongeza beki wa kati, beki wa kulia na kipa pekee.
“Lakini baada ya Mkude kutudengulia
kusaini mkataba, tumeona ni bora tukamsajili kiungo mwingine mwenye uwezo kama
wake, hatutaki tuwe na mchezaji mmoja tegemeo kwenye timu,” alisema bosi huyo.
Zacharia Hans Poppe ambaye ni
mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, akizungumzia hatua hiyo, alisema:
“Tunaendelea kufanyia kazi ripoti tuliyokabidhiwa na kocha wetu, hayo mengine
tutaangalia baadaye.”
Awali, Mkude aliliambia gazeti hili
kwamba, hajawahi kuzungumza na viongozi wake kuhusu mkataba mpya na anashangaa
kuhusu kuelezwa kwamba hapatikani hewani.
Kuhusu kuwazimia simu viongozi wa
Simba, Mkude alisema: “Ndiyo nilizima simu kwani wao walisema mimi nimeshasaini
mkataba mpya wakati si kweli, hivyo nikawa napata usumbufu kwa ndugu wengine
wakitaka kujua sababu za mimi kufanya hivyo bila kuwashirikisha na wengine
waliniomba fedha wakati si kweli. Haikuwa haki.”
Usajili wa dirisha dogo unaoendelea
sasa, ulianza Novemba 15, mwaka huu na unaisha Desemba 15.
Post a Comment