WAKATI Yanga
kuanzia benchi la ufundi hadi mashabiki wakitembea vifua mbele kujinadi kwa
kunasa kiungo mkabaji, Mzambia, Justine Zullu ambaye amepachikwa jina la Mkata
Umeme, Rais wa Simba, Evans Aveva, amemtupia dongo kwamba si lolote kwa kiungo
wao, James Kotei raia wa Ghana, aliyempachika jina la Mzima Swichi.
Ghafla Zullu
amekuwa gumzo hata kabla ya kucheza mchezo wowote ingawa juzi Jumamosi alicheza
dakika 45 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar ambao Yanga
ililala mabao 2-0.
Katika mchezo
huo, Mzambia huyo alionekana kuwa mzuri kwa pasi fupi na ndefu, mwenye umakini
lakini tatizo ni ‘slow’ kwenye kusaka mpira na hakabi.
Hata hivyo,
Aveva amewataka mashabiki na wanachama wa Simba ‘kumpuuzia’ kwani kiboko yake
ni Kotei anayehimili kiungo cha kukaba ili akasaidiane na Jonas Mkude kwenye
idara hiyo.
Bosi huyo
aliyasema hayo jana kwenye mkutano mkuu wa dharura wa klabu uliofanyika kwenye
Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar ambao ulilenga kubadili baadhi
ya vipengele vya katiba ya sasa.
Kauli ya
Aveva ilikuja wakati akielezea mikakati ya usajili kuelekea raundi ya pili
itakayoanza kutimua vumbi Desemba 17, mwaka huu.
“Kamati
zinafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunaboresha kikosi kama benchi la
ufundi lilivyopendekeza. Tayari tumemleta kipa (Daniel) Agyei na (James) Kotei
wote kutoka Ghana huyu ni kiungo mkabaji.
“Nasikia
wenzetu (Yanga) wanasema wamesajili mkata umeme (akimaanisha Zullu), sasa kwa
huyu wetu Kotei atakuwa mzima ‘Main Swich’,” alisema huku ukumbi uliobeba watu
642 ukilipuka kwa makofi na shangwe nyingi.
Tayari Kotei
yupo kambini na juzi Ijumaa alicheza kwenye mchezo wa kirafiki ambao Simba
iliifunga Poliso Moro mabao 2-0, huku leo huenda akatumika tena kwenye mchezo
wa kirafiki dhidi ya Mtibwa utakaopigwa Chamazi Complex.
Post a Comment