SIMBA imeandaa mkataba wa miaka miwili
ili impe kipa mpya Mghana, Daniel Agyei, lakini imekwama kufanya lolote hadi
kocha wake, Joseph Omog atakapotua nchini na kubariki usajili huo.
Kipa huyo, alitua nchini juzi Jumatano
akiwa na mabegi manne kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kusaini mkataba wa
miaka miwili Simba ili aweze kuichezea kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara
utakaoanza Desemba 17, mwaka huu.
Ujio wa kipa huyo, unaifanya Simba
kuwa na makipa wane, wengine wakiwa ni Muivory Coast, Vincent Angban, Peter
Manyika Jr na Denis Richard.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
timu hiyo, Zakaria Hans Poppe, alisema Mghana huyo wakati wowote atasaini
mkataba huo wa kuichezea Simba mara tu atakapotua Omog.
Hans Poppe alisema, hivi sasa wapo katika
hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kipa huyo watakayemsajili kwa ajili
ya kuleta ushindani wa namba kwenye timu.
Aliongeza kuwa, hadi hivi sasa
hawajajua mchezaji yupi atakayeachwa na kusajiliwa na hayo yatajulikana mara
baada ya kocha wao atakapotua nchini wakati wowote.
“Ni lazima tumsajili Agyei kutokana na
uwezo mkubwa alionao kwa ajili ya kumpa changamoto Angban katika nafasi hiyo ya
golikipa, na hayo ni mapendekezo ya kocha.
“Angban hakuwa na changamoto kutoka
kwa makipa wa akiba waliokuwepo kwenye benchi, hivyo ujio wake ninaamini
utaongeza changamoto na ushindani wa namba.
“Hivyo, hivi sasa tunamsubiria kocha
tu na mara atakapotua nchini, basi tutampa mkataba wa miaka miwili ya kuichezea
Simba,” alisema Hans Poppe.
Post a Comment