BEKI wa
Yanga, Mtogo, Vincent Bossou, amefunguka kwamba amerudi nchini kumalizia
mkataba wake wa miezi sita, kabla ya kuondoka moja kwa moja.
Anadai
kuwa awali aliomba kuununua mkataba huo lakini viongozi wa Yanga wakamuwekea
ngumu kwa kumgomea na kumtaka aje amalizane nao ndipo aondoke.
Bossou
ni miongoni mwa nyota wa kimataifa ambao mikataba yao inaelekea ukingoni akiwa
sambamba na Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima ambapo tayari
yeye ameweka bayana kwamba hataendelea kuichezea timu hiyo baada ya kupata timu
nje ya nchi.
Beki
huyo mwezi Januari, mwakani anatarajia kushiriki Kombe la Mataifa Afrika
(Afcon) litakalofanyika Gabon, ameliambia Championi
Ijumaa, kuwa amerejea siyo kwamba
amefeli majaribio nchini Vietnam kama inavyodaiwa bali anaheshimu mkataba
uliobakia na timu hiyo ambapo amepanga kuumaliza kabisa ili awe mchezaji huru
na aondoke bila ya kukorofishana na mtu.
“Sijafeli
majaribio Vietnam kama watu wanavyosema, ikumbukwe kwamba mimi nimecheza kule
miaka minne mfululilizo kabla ya kuja Yanga, sasa naendaje kufanya majaribio?
“Nimerudi
Yanga kwa ajili ya kumalizana na timu yangu kwa sababu viongozi hawakutaka
niondoke kwa kipindi sasa kutokana na msaada ambao nimeuonyesha kwenye mzunguko
wa kwanza na kwenye mechi za kimataifa.
“Niliwaomba
viongozi niweze kununua sehemu ya mkataba uliobakia na nilikuwa tayari kuwalipa
Yanga kiasi chochote ambacho wangehitaji, lakini wakagoma na kunitaka nije na
ndiyo nimerejea, nitacheza hadi pale mkataba wangu utakapoisha kwa sababu
naheshimu mkataba nilionao sasa lakini ukifika mwisho tu hawataweza kunizuia
kwa njia yoyote ile,” alisema Bossou.
Post a Comment