AKIANZA vema kibarua chake
kwa ushindi kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga,
Mzambia, George Lwandamina, ameleta kitu kipya kwenye timu hiyo.
Yanga ilipata ushindi huo
wakati timu hiyo ilipopambana na JKT Ruvu katika mechi ya ligi kuu
iliyomalizika kwa timu hiyo kushinda mabao 3-0 Uwanja wa Uhuru jijini Dar es
Salaam.
Ushindi huo, uliipeleka
Yanga kileleni na kuongoza kwenye msimamo wa ligi kuu wakifikisha pointi 36
huku ikiipita Simba iliyokuwa na pointi 35 kabla ya mechi dhidi ya Ndanda FC
iliyochezwa jana Uwanja wa Nangwanda Sijaona
huko Mtwara.
Katika mechi hiyo, Championi
Jumatatu lilimshuhudia kocha wa viungo wa timu hiyo, Mzambia, Noel Mwandila,
kwa mara ya kwanza akiwafanyisha mazoezi wachezaji wa kikosi cha
kwanza mara baada ya kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Mwandila akiwa na Lwandamina
waliwapangia koni wachezaji hao na kuwataka kukimbia mbio fupi huku wakiruka
koni kabla ya kuanza kipindi cha pili cha mchezo huo.
Yanga walifanya programu
hiyo ya muda mfupi ya dakika tano mara baada ya kuwahi uwanjani kabla ya
wapinzani wao Ruvu kuingia uwanjani kuanza pambano hilo.
Wakiendelea na programu hiyo
ambayo ni mpya na haijawahi kuwepo Yanga, waamuzi wa mchezo huo walimfuata
Mwandila na kumtaka kusitisha programu hiyo huku akiwataka wachezaji wajipange
kwa ajili ya mchezo huo.
Post a Comment