MSALA uliomkuta mwamuzi, Martin Saanya kwa kuchezesha mchezo wa Oktoba Mosi kati ya Simba na Yanga, umezua mapya, baada ya mechi ijayo itakayopigwa Februari 18, mwakani kuachwa pengo katika ratiba ya waamuzi kwa duru ya pili.
Ratiba hiyo ilipangwa tangu Desemba 5, mwaka huu na Chama cha Waamuzi Tanzania (Frat), kabla ya Jumapili iliyopita kupitishwa rasmi na Kamati ya Waamuzi, lakini mechi ya Simba na Yanga ikawekewa nyota kwa kile kilichosemekana ni kutokana na mechi zao kugubikwa na utata mkubwa, hivyo mwamuzi atatajwa baadaye.

Mmoja wa mabosi mhusika katika upangaji wa ratiba hiyo ya waamuzi, amelithibitishia Championi Jumatano na kutaja sababu kuu tatu ambazo zimewafanya waiweke chemba kwanza.
“Kwanza ni presha, maana mara nyingi mechi zao huwapa presha kubwa waamuzi, hasa wakijulikana mapema, pili tunataka tuwe makini zaidi katika kumpangia mwamuzi mechi hii kutokana na malalamiko mengi ambayo hutokea baada ya mchezo, hatutaki yaliyojitokeza Oktoba Mosi yajirudie.
“Pia tunataka kuanza tujiridhishe katika maamuzi ya mechi hizi nyingine, tuone yupi anayeweza kusimama katikati siku hiyo, ndiyo maana ikawekewa nyota,” alisema bosi huyo aliyeomba hifadhi ya jina na kusisitiza hata kamisaa wa mchezo huo hajapangwa.
Akina Saanya wamefungiwa miaka miwili kwa kosa la kuvurunda kwenye mchezo huo kwa kukataa bao halali la Ibrahim Ajibu wa Simba na kukubali bao la mkono la Amissi Tambwe pamoja na kadi nyekundu aliyopewa Jonas Mkude wa Simba iliyokuja kufutwa kwani haikuwa halali.


Post a Comment

 
Top