SIMBA inaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya kocha
mkuu wa timu hiyo Mcameroon, Joseph Omog na jana ilimshusha beki wa pembeni
Mnyarwanda, Niyonkuru Djuma anayekipiga Rayon Sports ya nchini huko.
Ujio huo ni katika mwendelezo wa kuifanyia kazi ripoti ya
Omog aliyoiacha kabla ya Ligi kuu Bara kusimama ambapo alipendekeza usajili wa
beki wa kulia katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 15 na
linatarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu.
Mchezaji huyo ambaye jana alitarajiwa kuanza mazoezi na
wenzake wa Simba anakuwa ni mgeni wa pili kwa timu hiyo ambayo juzi Jumatano
ilimshusha kipa namba moja wa Medeama ya Ghana, Daniel Agyei kwa ajili ya
kufanya naye mazungumzo ya kumsajili.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Ijumaa limezipata
ni kuwa beki huyo anayemudu kucheza namba zote za pembeni za ulinzi, alitua
nchini kimyakimya na kufikia kwenye moja ya hoteli kubwa iliyopo Sinza jijini
Dar es Salaam.
Imefahamika kuwa jana jioni alikuwa na ratiba ya mazoezi kwenye
Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kirwa Road wanapofanya Simba chini ya Kocha Msaidizi
Jackson Mayanja.
“Tumempokea beki mpya anayeweza kucheza nafasi zote za
pembeni namba mbili na tatu, anaweza kucheza hata katikati kama kocha akiamua
kumtumia kwenye nafasi hiyo.
"Ataanza mazoezi leo jioni (jana), akionyesha uwezo
mzuri basi tutampa mkataba kwa sababu kocha anahitaji beki wa pembeni namba
mbili," alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa kiungo wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna
Niyonzima na kuulizwa juu ya mchezaji huyo, alisema:
"Namfahamu vizuri Niyonkuru, nilikuwa naye timu ya
taifa ya Rwanda, ni mchezaji mzuri na mpambanaji, kama akisaini Simba watakuwa
wamepata mchezaji mzuri, nimesikia yupo hapa Tanzania ila sijajua zaidi kwa
kuwa sijawasiliana naye.”
Post a Comment