KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi
za Wachezaji chini ya Makamu Mwenyekiti, Raymond Wawa, inatarajiwa kukutana leo
kujadili na kutoa uamuzi wa mwisho wa suala la malalamiko ya klabu ya Simba juu
ya madai ya mchezaji wao, Hassan Ramadhani ‘Kessy’, aliyetimkia Yanga.
Mara ya mwisho kamati hiyo kukutana
ilikuwa mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo pamoja na mambo mengine, iliiagiza
Simba kuwasilisha vielelezo vya kumlipa Kessy mishahara ya miezi mitatu ya
mwisho kabla ya kumalizika mkataba wake.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka
nchini (TFF), Alfred Lucas, aliliambia DIMBA kuwa shauri hilo litasikilizwa leo
na huenda kamati ikatoa maamuzi ya mwisho, kwani Simba walishawasilisha
vielelezo hivyo katikati ya wiki hii.
“Kamati husika inayosimamia suala
hilo itakutana mapema kesho (leo) kujadili suala hilo na kulitolea maamuzi, kwa
vile kila kitu kiko mezani, ikiwamo vielelezo kutoka Simba,” alisema.
Simba inailalamikia Yanga kumsajili
Kessy, akiwa bado ni mwajiriwa wao halali, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi
wanawataka Yanga kulipa Sh milioni 200, jambo ambalo wanajangwani wanalipinga.
Awali kamati hiyo iliwapa muda Simba
na Yanga kukaa meza moja ili kujadiliana kindugu na kuyamaliza, lakini hakuna
lililofanikiwa na sasa kamati hiyo imeamua kulimaliza kwa mujibu wa sheria na
kanuni zilizopo.
Post a Comment