WAKATI mvutano juu ya uhalali wa beki Hassan Kessy ukiendelea, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema iwapo Simba itafanikiwa kushinda kesi hiyo, bado Yanga haitapoteza pointi katika mechi ambazo Kessy amecheza.

Suala la Kessy limekuwa likiibua maswali na mvutano kwa muda mrefu tangu msimu uanze na bado halijapatiwa utatuzi kutokana na kutoafikiana baina ya klabu hizo.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, alisema Simba haikumtolea pingamizi Kessy bali kesi yao ni ya madai, kama wangefungua kesi ya pingamizi, hapo ndipo suala la pointi lingeibuka.

“Mkataba wa Kessy na Simba ulimalizika Juni 15 na tarehe 27 ndiyo waliwasilisha barua ya kuilalamikia Yanga kuzungumza na mchezaji wao lakini siyo kwamba aliingia mkataba lakini ikumbukwe kuwa wakati wanasema hivyo, tayari mkataba wao na mchezaji ulikuwa umeshakwisha.

“Hivyo kwa sasa kesi ambayo inaendelea TFF ni kati ya Yanga na Simba ya madai ya kuzungumza na mchezaji lakini kwa upande wa mchezaji, hahusiki kabisa na suala hilo kwa kuwa alikuwa ameshamaliza mkataba na timu yake hiyo.

“Iwapo itatokea Simba ikashinda kesi, basi Yanga haiwezi kupokwa pointi kwa kuwa hawakumwekea pingamizi hata kidogo katika usajili uliopita licha ya kutoa malalamiko hayo yote, hivyo mchezaji ataendelea kuwa mali ya Yanga na kilichopo hivi sasa ni suala la madai tu.

“Kinachoendelea hivi sasa ni kama vile mtu analalamikia kuhusu mke wake kurubuniwa na jamaa mwingine huku kwa upande wake akiwa hayupo naye kwa kipindi hicho huyo mke ila kinachobakia ni madai kuwa alimrubuni mke wake na kusababisha kuachana hivyo kuwepo kwa kesi ya madai tu.

“Kwa sasa kesi inaendelea vizuri na ipo katika hatua nzuri ya kuweza kufikia mwisho hivyo tukizungumza sana tunaweza tukavuruga kile kinachoendelea na wakati wowote kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Mwesigwa.


Post a Comment

 
Top