STRAIKA mpya wa Simba, Juma Luizio, aliyetua kwenye usajili wa dirisha dogo uliofungwa juzi Alhamisi, ameweka bayana kwamba lengo lake ni kuhakikisha anaingia katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kuwaweka nje wachezaji wenzake, Laudit Mavugo na Frederic Blagnon.
Usajili wa Luizio aliyetua Simba kwa mkopo wa miezi sita akitokea Zesco ya Zambia, ni agizo la kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog ambaye alikuwa anahitaji mshambuliaji kwa ajili ya kuliongezea nguvu eneo hilo.

Luizio aliyewahi kuwika na Mtibwa Sugar kabla ya kwenda Zambia, ameliambia Championi Jumamosi kuwa licha ya kutambua ugumu wa namba ndani ya kikosi hicho, kwake amejipamga vilivyo kuhakikisha anapata namba ndani ya kikosi cha kwanza.
“Najua kwamba ushindani wa namba ni mkubwa hapa Simba lakini nikuhakikishie kwamba lazima niingie ndani ya kikosi cha kwanza kwa sababu natambua uwezo wangu ulivyo.
“Nimekuja kufanya kazi hapa, hivyo natakiwa  kupambana kutimiza majukumu yangu na namuomba Mungu anisaidie niweze kutimiza malengo niliyojiwekea, ikiwemo kuipa ubingwa Simba,” alisema Luizio.

Post a Comment

 
Top