RAIS wa Simba SC, Evans Aveva amewahakikishia wanachama wa klabu hiyo kuwa wanasajili fowadi mmoja tu ili wafunge mahesabu ya usajili lakini wachezaji wawili wanaweza kwenda na maji kabla ya kufungwa dirisha usiku wa kuamkia Ijumaa hii.
Aveva aliyasema hayo kwenye Mkutano Mkuu wa Dharura wa wanachama uliofanyika jana kwenye Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa akielezea mwelekeo na maandalizi ya raundi ya pili.
Aveva alisema katika kuhakikisha wanabakia kileleni, tayari wamemnasa kipa na kiungo mkabaji na kusisitiza kuwa katika mapendekezo ya kocha, Joseph Omog anahitajika straika mmoja mzawa na kuondoa baadhi ya wachezaji kwenda kwa mkopo.
Akaweka wazi kuwa tayari wameachana rasmi na beki Malika Ndeule na kusisitiza wengine wawili wapo njiani kabla ya Desemba 15, mwaka huu siku ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
“Tulikaa na kocha kutaka kujua kilichosababisha tupoteze mechi za mwishoni (dhidi ya African Lyon na Prisons), akaeleza kwamba anahitaji kuimarishiwa golini na safu ya ushambuliaji.
“Tayari kipa amepatikana (Mghana, Daniel Agyei) na tukamuongezea kiungo James Kotei na bado kamati ya usajili iko sokoni kutafuta mshambuliaji mmoja kama alivyotaka kocha na atapatikana kabla ya dirisha kufungwa.
“Lakini pia wachezaji watatu tumeona ni heri kuwatoa kwa mkopo. Tayari Malika tumemalizana naye na wengine wawili wataondoka muda wowote,” alisema Aveva.
Katika hatua nyingine, Aveva akasisitiza kupuuzwa kwa taarifa zinazozidi kuzagaa kila kona juu ya wao kumalizana na kiraka aliyetemwa na Yanga, Mbuyu Twite juzikati.
Bosi huyo akatupa dongo kwamba katu Simba haiwezi kusajili kutoka Yanga, badala yake wao ni kama akademi ambayo Yanga lazima wakimbilie kuchukua wachezaji.

Post a Comment

 
Top