BAADA ya Simba
kushindwa kumalizana na kiungo wake, Jonas Mkude juu ya kumwongezea mkataba
mpya, nyota huyo amezua balaa jipya klabuni hapo ambapo ameugawa uongozi.
Viongozi wa Simba
wanadaiwa kugawanyika makundi mawili juu ya mchezaji huyo ambapo baadhi yao
wanataka aachwe baada ya mkataba wake kuisha lakini wengine wanataka aongezwe
mkataba mpya.
Habari za kuaminika
katoka ndani ya Simba zimedai kuwa viongozi wanaotaka Mkude aondoke ni wale
ambao wanaamini kiungo James Kotei kutoka Ghana anaweza kuziba pengo la Mkude.
“Wale wanaotaka
Mkude abaki wanaona kuwa Kotei hana uwezo wa kumshinda Mkude, hivyo endapo
watamuacha aondoke basi pengo lake litawachukua muda mrefu kuliziba.
“Hali hiyo imefanya
mpaka sasa Mkude kutopewa mkataba mpya licha ya matatizo yote yaliyojitokeza
hapo awali kati yake na uongozi kuwa tayari yameshapatiwa ufumbuzi,” kilisema
chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa Mkude
kuhusu mkataba mpya, alisema: “Sijasaini na mpaka sasa sijui chochote
kinachoendelea lakini hilo haliniumizi kichwa kwani mimi nafanya kazi yangu
uwanjani.
“Inawezekana kuna
mambo hayajakamilika lakini mimi sina tatizo watakaponiletea mkataba nitausaini
kama utakidhi yale yote ambayo tulikubaliana.”
Alipotafutwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe hakupatikana,
Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele hakupokea simu lakini Makamu wa Rais wa
klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema: “Sielewi lolote kuhusu suala
hilo.”
Post a Comment