SARE ya bao 1-1 waliyoipata Yanga jana dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru, imezidi kuwafanya wapenzi wa Simba kubaki wakicheeka wakiamini matokeo hayo yamewapa ahueni katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Matokeo ya mchezo huo, yamepunguza kasi ya Yanga na kufanya pengo kuwa la pointi moja na kwamba iwapo Simba itaichapa JKT Ruvu leo kwenye uwanja huo, jijini Dar es Salaam, itafikisha pointi 41 na kuwaacha watani wao hao waliopo nyuma yao kwa pointi nne.
Na habari njema kwa wapenzi wa Simba ni kwamba uongozi wao umeshalimaliza tatizo la vibali vya kazi kwa wachezaji wao wa kigeni hivyo leo watajumuika na wenzao kusaka pointi tatu ili waendelee kujinafasi kileleni mwa ligi hiyo.
Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema hawataki kurudia makosa yaliyojitokeza kwenye mzunguko wa kwanza walipotoka suluhu na JKT Ruvu na badala yake watahakikisha wanashinda.
“Tulipokutana mzunguko wa kwanza tulitoka 0-0 na sasa tunakwenda kukutana tena nao, imani yangu ni kwamba tutafanya vizuri na kuondoka na pointi zote tatu ili tuzidi kukaa juu,” alisema.

Wekundu wa Msimbazi hao wana misimu minne mfululizo bila kunusa harufu ya ubingwa na kushindwa kabisa kushiriki michuano ya kimataifa ikiziangalia Yanga na Azam FC zikibadilishana nafasi za juu.
Tangu msimu huu uanze, Simba wameonekana wazi kupania kutwaa ubingwa huo kutokana na kandanda wanaloonyesha, lakini pia matokeo mazuri wanayoyapata na hivyo kuelekea kuwarejeshea mashabiki wao furaha waliyoikosa kwa muda mrefu.

Post a Comment

 
Top