JUZI Jumamosi baadhi ya viongozi wa Simba walijitokeza katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kirafiki kati ya Yanga dhidi ya JKU ya Zanzibar.
Lengo kubwa la viongozi hao kufika uwanjani hapo ni kumuona kiungo mpya wa watani wao wa jadi, Yanga raia wa Zambia, Justine Zulu ambaye amepachikwa jina la ‘Mkata Umeme’.
Katika mchezo huo ambao Yanga ilichezesha vikosi viwili, ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kuwa Zulu waliyemuona uwanjani si yule waliyekuwa wakisikia sifa zake kupitia vyombo vya habari.

Alisema ni mchezaji wa kawaida sana kama walivyo wachezaji wengi wa hapa nchini na hata hilo jina la Mkata Umeme haliendani naye.
“Nilikuja hapa uwanjani kwa ajili ya kumuona huyo Mkata Umeme wa Yanga, lakini sijaona kitu cha ajabu kutoka kwake.
"Ni mchezaji wa kawaida sana na ni matumaini yangu siku akikutana na viungo wetu atapata shida lakini pia siku hiyo Yanga ndipo watakapomkumbuka Mbuyu Twite," alisema Kaburu.

Post a Comment

 
Top