BAADA ya kumwaga wino wa kuichezea
Yanga, kiungo mkabaji wa timu hiyo, Justine Zulu amekabidhiwa jezi namba 14
ambayo inaelezwa kuwa na mkosi.
Jezi hiyo, ina sifa moja pekee ambayo
kila mchezaji mpya atakayeivaa huwa hadumu kwenye timu muda mrefu na badala
yake kujikuta anatemwa au kuanza na wakati mgumu.
Kati ya wachezaji waliowahi kuivaa
jezi hiyo na kudumu kwa kipindi kifupi ni kiungo mshambuliaji raia wa Niger,
Issofou Boubacar aliyedumu na timu hiyo kwa miezi sita pekee kwenye msimu wa
2015/2016, pia beki wa kati Rajab Zahiri aliyeitumikia kwa msimu mmoja na nusu.
Zulu anayefahamika pia kama mkata
umeme kutokana na sifa yake ya uhodari wa kukaba na kuanzisha mashambulizi,
yeye mwenyewe ndiye aliyeomba apatiwe jezi hiyo.
Zulu, raia wa Zambia, ataitumia jezi
hiyo kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika
mwakani.
“Zulu amepewa jezi namba 14 mara tu
baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Yanga, ataanza kuonekana
nayo kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu.
“Jezi hiyo, yeye mwenyewe ndiye
aliyeiomba kabla ya viongozi kumpa na kuanza kuivaa kwenye mazoezi ya leo
(jana) jioni kwenye viwanja vya Gymkhana,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa meneja wa timu hiyo,
Hafidh Saleh kuzungumzia hilo, alisema: “Hizo taarifa ni za kweli, Zulu nimempa
jezi namba 14 aliyoiomba yeye mwenyewe.
“Nilimpa jezi namba 18 iliyokuwa
inavaliwa na Domayo (Frank) na baadaye Tinoco (Benedicto), nyingine ni namba mbili
iliyokuwa inavaliwa na Telela (Salum) na 29 aliyokuwa anaivaa Godfrey Mwashiuya
ambaye sasa anavaa 19 na 14 lakini yeye akachagua 14,” alisema Saleh.
Post a Comment