SIKU chache
baada ya Simba kutakiwa vithibitisho vya kumlipa mishahara beki wake wa zamani,
Hassan Ramadhani ‘Kessy’, Wekundu hao wa Msimbazi wameibuka na kusema wana kila
karatasi iliyotakiwa kwenye sakata hilo.
Simba
iliombwa uthibitisho huo kufuatia hoja iliyowasilishwa na Mwanasheria wa Yanga,
Alex Mgongolwa, katika kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, kwamba
Simba haina uhalali wa madai yoyote dhidi ya Kessy kwa sababu haikumlipa
mshahara kwa miezi mitatu.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope, alisema wana uthibitisho wote
uliotakiwa na kamati hiyo itakayokaa wikiendi hii.
Alipoulizwa
kama wana uthibitisho na vielelezo, Hans Pope alijibu kifupi sana: “Yap vipo,
Yanga hawana hoja wanatapatapa tu.”
Katika kikao
cha awali kilichofanyika Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Yanga walidai kwamba Simba hawakumlipa mchezaji huyo kwa miezi mitatu kuelekea
mwisho wa mkataba wake na kwa mujibu wa sheria, hawana haki ya madai yoyote
dhidi yake.
Yanga
waliiomba Kamati ipokee vithibitisho vya vielelezo vya kupelekwa mishahara ya
Kessy kwenye akaunti yake ya benki na si vinginevyo, kwa kuwa wana wasiwasi
wapinzani wao wanaweza kufoji nakala za kumlipa mkononi.
Simba
inalalamikia klabu ya Yanga kumsajili beki Kessy akiwa hajamaliza mkataba wake
Msimbazi na kwa sababu hiyo inataka kulipwa Sh milioni 200 ambayo ni punguzo
kutoka bilioni 1.2 walizozitaka awali.
Post a Comment