HATIMAYE siri
kubwa imefichuka kuwa mgomo wa Yanga una kitu kikubwa nyuma yake.
Wachezaji wa
Yanga juzi na jana waligoma kufanya mazoezi asubuhi kwa kile kinachodaiwa kuwa wanashinikiza
ili walipwe fedha zao za mshahara wa mwezi Novemba, lakini pia ikielezwa kuwa
wanataka malipo yao ya mwezi huu mapema kwa sababu ya sikukuu.
Hata hivyo,
Championi limechimba na kugundua kuwa kuna siri nyingine nyuma ya ishu hiyo ya
mishahara kwani wachezaji wa timu hiyo hawataki mazoezi magumu ya kocha wao
mpya George Lwandamina.
Wachezaji wa
Yanga wamekuwa wakilalamika chinichini kuwa mazoezi ya kocha huyo ni magumu
sana, lakini wakati mwingine amekuwa akiwafanyisha kwenye jua kali jambo ambalo
linawaumiza.
Inaelezwa kuwa
wachezaji hao wamekuwa wakimweleza mmoja kati ya mabosi wa timu hiyo jina
(tunalo), kuhusu mazoezi ya kocha huyo raia wa Zambia lakini amekuwa akiwaeleza
kuwa hana cha kufanya jambo ambalo liliwafanya watumie kundi lao la mtandao wa
WatsApp kupeana taarifa za kugomea mazoezi hayo ambayo walitakiwa kuyafanya
juzi jioni na jana.
“Ishu hapa siyo
mishahara, kwa Yanga kugoma kwa ajili ya mishahara ni jambo gumu kwa kuwa kuna
wakati mwingine wachezaji huwa wanalipwa hata miezi ambayo hawajaifanyia kazi
na wakati mwingine wanapewa posho mbalimbali kuliko hata klabu nyingine.
“Ishu hapa bwana
ni mazoezi, wachezaji wamekuwa hawapendezwi na mazoezi ya kocha huyo, wamekuwa
wakisema mara kwa mara lakini wanakosa msaada hivyo wameamua kugoma wenyewe,
wanaamini njia hii inaweza kuwasaidia kocha huyo akaelezwa akaelewa, waliwahi
kushtaki kwa bosi mmoja (jina tunalo) lakini akawaeleza kuwa hana la kufanya,”
kilisema chanzo cha uhakika toka ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo,
tofauti na juzi ambapo wachezaji walifika kwenye Uwanja wa Uhuru na kugoma
kuingia uwanjani, jana asubuhi hawakufika kabisa huku viongozi wa benchi la
ufundi wakifika uwanjani hapo na kukaa kwa muda kabla hawajawasha basi lao na
kutimka.
Taarifa zimekuwa
zikisema kuwa mgomo huo unawahusisha wachezaji wote isipokuwa kiungo mpya wa
timu hiyo Justine Zulu, ambaye yeye alishamzoea kocha huyo hivyo haoni shida
ndiyo maana amekuwa akifika mazoezini hapo akiwa na vifaa vyake.
Pamoja na kwamba
uongozi wa Yanga jana ulisema wachezaji hao watamaliziwa matatizo yao wakati
wowote upande wa Lwandamina yeye alitupia malalamiko kwa wachezaji kupitia
ukurasa wake wa kijamii wa Facebook akiandika :"Habari za asubuhi marafiki
zangu, soka la kulipwa linahusishwa na nidhamu, hivyo ni lazima kuwa makini
"Hakuna
mchezaji atakayeweza kufanikisha ndoto zake bila ya kufanya mazoezi, mazoezi ni
kitu muhimu hatakama yanapotokea matatizo, huo ndiyo mwongozo mzuri katika
kupata mafanikio ya mchezaji,"aliandika Lwandamina.
Pamoja na mazoezi
hayo mechi ya kwanza ya kocha huyo dhidi ya JKT Ruvu Yanga walishindwa kwa
mabao 3-0.
Post a Comment