SARE ya bao 1-1 iliyopata Yanga dhidi ya African Lyon, jana ilikuwa chungu na kusababisha hali ya sintofahamu baada ya baadhi ya mashabiki wa Yanga kukasirishwa na matokeo hayo na kuzua varangati kiasi kwa wachezaji wa timu hiyo.

Matokeo hayo ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara ambayo yanaifanya Yanga iendelee kubaki nafasi ya pili katika msimamo wa hiyo kwa kufikisha pointi 37 nyuma ya Simba yenye pointi 38, yaliwakasirisha baaadhi ya mashabiki walioamini kuwa wachezaji wao walifanya uzembe na ndiyo maana waliambulia pointi moja katika mchezo huo.

Wakati akitoka uwanjani hapo akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Altezza, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva alisimama pembeni kidogo ya barabara, ghafla askari wa usalama barabarani walimfuata na kumwambia amesimama sehemu ambayo hatakiwi kuegesha gari.

Msuva akajitetea kuwa alikuwa akimsubiri mchezaji mwenzake, Ramadhani Kessy ambaye kweli alifika baada ya dakika kadhaa lakini askari hao hawakumuelewa, badala yake wakamtaka aende kituoni au alipe faini ya Sh 30,000.

Kuona hivyo, mashabiki wakaongezeka kwa wingi eneo hilo la tukio na kuwabembeleza askari hao lakini msimamo ulikuwa ni uleule, ndiyo wakalazimika kuchanga kiasi hicho cha fedha na kumlipia Msuva ndipo akaruhusiwa kuondoka huku akiwashukuru mashabiki hao.

Post a Comment

 
Top