KUMBE kiungo mpya wa Yanga raia wa Zambia, Justine Zulu ‘Mkata Umeme’ alikuwa amepangwa kuwemo katika kikosi kilichoivaa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru juzi lakini jina lake likakatwa dakika za mwisho, likiwa tayari limeandikwa kwenye karatasi ya majina ya wachezaji wa mchezo husika ‘line up’.


Mashabiki wa Yanga walitarajia kumuona kiungo huyo akianza kuonyesha ufundi wake katika mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara lakini badala yake akaishia kukaa jukwaani.

 Zulu amejiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Klabu ya Zesco ya nchini kwao.

Kocha wa Makipa wa Yanga, Juma Pondamali, amesema Zulu alipaswa acheze kwenye mchezo huo lakini ilishindikana dakika za majeruhi, baada ya benchi la ufundi na uongozi wa timu hiyo kugundua kuwa kulikuwa na baadhi ya taratibu za nchi hazijatekelezwa, hivyo nafasi yake ikachukuliwa na Said Makapu ambaye alikuwa hajapangwa kucheza siku hiyo.

Pondamali alisema muda mfupi kabla ya mchezo huo uliomalizika kwa Yanga kushinda 3-0, benchi la ufundi lilikata jina la Mkata Umeme baada ya kuonekana hawezi kucheza kutokana na kutokuwa na kibali cha kufanyia kazi na kile kinachomruhusu kuishi hapa nchini.

“Kweli Zulu amekatwa jina lake tukiwa uwanjani kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na nafasi yake ikachukuliwa na Makapu ambaye awali alikuwa hajapangwa kwenye kikosi kabisa.

“Kocha Lwandamina tayari kwenye listi yake alikuwa ameshampanga, lakini ilibidi tubadilishe mwishoni baada ya kukaa na kujadiliana kwa kina na kugundua kuwa kama tungemchezesha wakati taratibu za nchi hazijakamilika basi tungeweza kumuingiza matatani bila sababu za msingi, hivyo njia rahisi tukaona ni vyema kumuondoa kabisa kwenye kikosi hadi taratibu zitakapokamilika.

“Nina imani kuanzia Jumatatu (leo) uongozi utaanza kushughulikia taratibu hizo na bila shaka kwenye mchezo wetu dhidi ya African Lyon tutaweza kumtumia, kwani leo (juzi) tumeulizwa sana swali hili na mashabiki wetu,” alisema Pondamali.

Tangu Ijumaa ya wiki iliyopita, Yanga ilikuwa tayari imeshapokea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji huyo kiasi cha kulifanya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwapatia baraka zote za kumtumia kiungo huyo ambaye anasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo.

Yanga itavaana na African Lyon Ijumaa ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na katika mchezo huo, ndipo mashabiki wanaweza kuyaona maufundi ya Mkata Umeme ambaye atatarajiwa kuwakatia umeme viungo wa Lyon katika dimba la kati, hatua ambayo itawafanya wazungukezunguke tu bila kuuona mpira kama wapo gizani vile!

Katika mazoezi ya mwishomwisho kabla ya mchezo dhidi ya JKT Ruvu ambao Yanga ilishinda 3-0, wachezaji wa Lyon waliokuwa wamemaliza mazoezi na kisha Yanga kuingia, walisikika wakimjadili Mkata Umeme baada ya kumuona akicheza na kukiri kwamba ni mchezaji hatari, hasa akizoea mazingira ya Tanzania.

Post a Comment

 
Top