KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, ameibuka na kusema kama kweli wanataka kuwa mabingwa msimu huu, ni lazima wawe makini katika kila mchezo wao ili kufikia malengo yao.
Omog ambaye huu ni msimu wake wa kwanza akiwa anaiona Simba aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu, katika mzunguko wa kwanza amefanikiwa kuiweka timu hiyo kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kujikusanyia pointi 35, mbili zaidi ya watani zao wa jadi, Yanga, wanaoshika nafasi ya pili.
Timu hiyo ambayo Jumapili ijayo itaanza kutupa karata yake ya mzunguko wa pili wa ligi kwa kucheza dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, juzi Jumatatu ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mtibwa ukiwa ni mchezo wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Mcameroon huyo, amesema: “Tunahitaji ubingwa wa ligi msimu huu, hivyo kwa kipindi hiki ni lazima tuwe makini kabla na baada ya mchezo, lengo likiwa ni kufikia kwenye malengo yetu hayo na mzunguko wa pili ndiyo unahitaji umakini wa kweli vinginevyo mambo yatakuwa magumu kwetu.”

Post a Comment

 
Top