WAKATI Baraza la Wadhamini la klabu ya Simba likiibuka na kusema Mkutano Mkuu wa wanachama uliopangwa kufanyika Desemba 11 mwaka huu ni batili, uongozi umekutana na matawi jana na kuafikiana kuwa hakutakuwa na mabadiliko yoyote.
Baraza hilo la Wadhamini kupitia kwa Mwenyekiti wake, Mzee Hamis Kilomoni, walisema mkutano huo ni kinyume cha katiba na kuitaka Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kuupiga marufuku.
Hata hivyo, Kamati ya Utendaji ya Klabu hiyo ikiongozwa na Rais wake, Evans Aveva walikutana na viongozi wa matawi ambapo pamoja na mambo mengine, waliafikiana kuwa mkutano wao upo palepale, kwani wameuitisha kikatiba.
Simba wapo kwenye mchakato wa kutaka kuifanyia katiba yao marekebisho ili kuruhusu mfumo mpya wa hisa, baada ya mfanyabiashara na mwanachama wao maarufu, Mohamed Dewji ‘Mo’ kuweka wazi kuwa anataka kuweka hisa ya asilimia 51 (51%).
Hata hivyo, Baraza la Wadhamini wanaona kwamba mkutano huo ni batili na wameweka wazi kuwa hawaungi mkono Mo kupewa hisa ya asilimia 51, wakidai kuwa atakuwa na sauti kubwa na anaweza kuifanya timu lolote, kwani ndiye atakayekuwa na mamlaka makubwa.

Post a Comment

 
Top