SIMBA, leo Jumamosi inacheza dhidi ya JKT Ruvu
katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wamesema hawana muda
wa kuiacha Yanga itambe kileleni mwa ligi hiyo badala yake imepanga kushinda
leo na kusonga mbele.
Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ilikuwa
na pointi 38, inataka iendelee kukaa kileleni kwa muda mrefu hadi itwae ubingwa.
Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja
amesema vijana wake wapo kwenye ari nzuri ya kuchukua pointi tatu leo, hivyo
anaamini wataendelea kupeta kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
“Kila mchezo tunataka kushinda ili kufikia malengo,
hatuna nafasi ya kuzembea na kuwaachia wapinzani wetu watuongoze.
“Tumejipanga kukabiliana nao hao JKT Ruvu kwani
tunajua katika mchezo wa awali walituzuia na kuondoka na pointi moja, lakini
safari hii hilo halitatokea, tutawafunga na kuondoka na pointi zote tatu,”
alisema Mayanja.
Kwa upande wa Kocha wa JKT Ruvu, Bakari Shime ambaye
katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga alikiongoza kikosi hicho kwa mara ya
kwanza na kuambulia kipigo cha mabao 3-0, alisema: “Vijana wangu wameniahidi
ushindi, kubwa zaidi wamesema watajituma kadiri wawezavyo kuhakikisha
hatupotezi mchezo wa pili mfululizo. Tunajua tupo kwenye hali mbaya, hivyo
itakuwa vizuri tukishinda mchezo huu.”
Ikumbukwe kuwa, JKT Ruvu ambayo inashika nafasi ya
pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 13, iliweza kuilazimisha suluhu Simba katika
mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar.
Post a Comment