Caf kuilipia Yanga mishahara
YANGA inahesabu siku tu kabla ya kuanza kuogelea mamilioni ya fedha za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) ambazo wakizitumia vema wanaweza kuondokana na tatizo la hivi karibuni la kuchelewa kuwalipa mishahara wachezaji wake pamoja na matumizi mengine ya klabu.
Ipo hivi. Kuanzia mwakani michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika itajulikana kama Total Caf Club Championship, chini ya udhamini wa kampuni ya mafuta ya Total, ambayo itatoa zawadi kwa timu shiriki kwa kila hatua.
Yanga itaiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo mwakani na kutokana na mabadiliko makubwa ya udhamini wa michuano hiyo, watakuwa wakiingiza mkwanja kila hatua.
Kama watafanya vizuri, fedha ambazo watakuwa wakizipata, zinaweza kuwasaidia kufanya mambo makubwa mengi na kuondoa matatizo mengi katika klabu hiyo.
Mwanzoni mwa wiki hii wachezaji wa Yanga waligoma kufanya mazoezi kwa siku mbili kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kucheleweshewa mishahara yao lakini sasa tatizo hilo linaweza kufika kikomo kama watajitahidi na kufika hatua nzuri michuano ya kimataifa.
Yanga wataianza michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua za awali wakicheza na timu ya Ngaya de Mbe ya nchini Comoro ambapo Wanajangwani hao wanapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi michezo yote miwili na kusonga mbele.
Ikiwa Yanga itafika katika hatua ya makundi katika michuano hiyo na kushika nafasi ya mwisho au ya tatu katika kundi itajipatia kiasi cha dola za Kimarekani 550,000 sawa na zaidi ya Sh bilioni moja na milioni 100.
Kama Wanajangwani hao watapigana kiume na kushika nafasi ya kwanza au ya pili katika kundi na kuingia robo fainali, bila shaka watafurahia maisha kwani watajipatia kiasi cha dola za Kimarekani 650,000 sawa na bilioni moja na milioni 300.
Na kama watapiga hatua kubwa zaidi na kuvuka hatua hiyo ya robo fainali ma kuingia nusu fainali maisha kwao yatakuwa mteremko kwani timu itajipatia dola za Kimarekani 800,000 sawa na bilioni moja na milioni 600 za Kitanzania.
Kama watapambana na kufika fainali na kwa bahati mbaya wakafungwa na kumaliza nafasi ya pili haitakuwa shida kwao kwani wataondoka na kitita cha dola za Kimarekani milioni moja na laki mbili na nusu sawa na bilioni mbili na milioni mia tano.
Ikiwa watatinga fainali na kutwaa kombe hilo, kwanza nchi italipuka kwa furaha kwani itakuwa ni historia ambayo haijawahi kutokea na pili watatajirika kwani wataondoka na dola za Kimarekani milioni mbili na laki tano sawa na Sh bilioni tano.
Hiyo inamaanisha kuwa kama wachezaji waliopo watajituma na kupata matokeo mazuri katika hatua hizo zote, bila shaka mishahara kwa Yanga itakuwa ni historia na badala yake watasikia tu kwa majirani zao wakilia.
Mbali na Yanga kujipatia fedha hizo, pia Shirikisho la Soka nchini (TFF) nao watafaidika kwani Wanajangwani hao wakifika hatua ya makundi shirikisho hilo litalamba dola 27,500 sawa na Sh milioni 55.
Wakifika robo fainali TFF watalamba dola 32,500 sawa na Sh milioni 65 na ikiwa watafika nusu fainali shirikisho hilo litaweka kibindoni dola 40,000 sawa na shilingi milioni 80 na ikiwa watamaliza nafasi ya pili TFF watalamba dola 62,500 sawa na milioni 125 na ikiwa Wanajangwani hao watakuwa mabingwa basi TFF watalamba dola 125,000 sawa na shilingi milioni 25.
Post a Comment