KLABU ya Simba imefanikiwa kumng’oa mshambuliaji wa Stand United, Pastory Athanas kwa dau la Sh milioni 15, imefahamika.
Athanas ni miongoni mwa wachezaji kadhaa waliotua Simba katika usajili wa dirisha dogo ambapo Simba imeshusha wachezaji wapya sita wakiwemo wawili waliopandishwa kutoka katika kikosi cha vijana.
Bosi kutoka Stand United amesema wameamua kumuachia mchezaji huyo kwa dau la Sh milioni 15 ambapo kulikuwa na mvutano katika usajili wake hadi kufikia dakika za mwisho pale klabu hizo zilipokubaliana.
“Tumemuachia Pastory kwa dau la milioni 15 ambalo ndilo uongozi ulikubaliana na viongozi wa Simba, ambapo mchezaji huyo alikuwa na mkataba, hivyo uongozi umeona ni vyema kumuondoa kwa dau hilo,” alisema bosi huyo.
Bosi mmoja kutoka Simba alieleza kuwa kutokana na hali iliyojitokeza katika usajili wa mchezaji huyo, ilibaki kidogo waachane naye kutokana na mvutano uliokuwepo baina ya timu hizo mbili hadi dakika za mwisho walipoamua kuwaachia.
“Usajili wa Pastory ulikuwa mgumu hadi dakika za mwisho uongozi wa Stand ulikuwa unasumbua kutoa barua ya kumruhusu, hivyo kusababisha kuchukua muda mrefu kujadili suala hilo hadi pale walipoidhinisha kutoa barua hiyo,” alisema bosi huyo.

Post a Comment

 
Top