TAYARI presha ya mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu Bara imeonekana kuanza kwa makocha wa timu mbili zinazofukuzana kwa
karibu kuuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Kocha George Lwandamina raia wa
Zambia na Joseph Omog raia wa Cameroon, hadi kufikia jana walikuwa bize
kuviandaa vikosi vyao kwa ajili ya mechi zao za kwanza za ligi hiyo
zitakazopigwa wikiendi hii lakini wote wawili wakagoma kuzungumzia chochote
kuhusiana na mitanange hiyo.
Yanga ndiyo itakayokuwa ya kwanza
kurusha karata yake itakapovaana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar
es Salaam leo Jumamosi wakati Simba italazimika kusubiri kwa saa 24 zaidi kabla
ya kuwavaa Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Kama Yanga wakishinda mchezo wa leo
Jumamosi watakaa kileleni na kuwatia presha wapinzani wao. Hadi sasa Yanga na
Simba zinazidiana kwa pointi mbili tu. Simba wapo kileleni kwa pointi 35,
wakati Yanga wapo nyuma yao wakiwa na pointi 33.
Hata hivyo, kwenye mazoezi ya Yanga
yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, jana asubuhi, Lwandamina alipotakiwa
kuzungumzia mchezo wake dhidi ya JKT Ruvu aligoma kabisa, badala yake akampa
nahodha Haruna Niyonzima majukumu hayo ya kuzungumza.
“Uongozi umenikataza kuzungumza hadi
pale utakaponipa ruhusa, ongeeni na wale kule (Niyonzima na Nadir Haroub
‘Cannavaro’),” alisema kwa ufupi Lwandamina alipofuatwa na waandishi wetu,
kisha akaelekea kupanda gari haraka na kuondoka.
Pia gazeti hili lilipomtafuta Omog
hakuwa akipokea simu kwa muda wote aliopigiwa jana, hatua ambayo imetafsiriwa
kuwa naye amegoma kuzungumza.
Gazeti hili linafahamu kuwa makocha
hao wapo kwenye presha kubwa kuelekea mechi hizo za kwanza, ndiyo maana siyo
wepesi kuzungumza.
Post a Comment