MSHAHARA mkubwa anaolipwa Mzambia, Obrey Chirwa
ndani ya Yanga, imeelezwa kuwa ndiyo sababu kubwa iliyoifanya klabu hiyo
kushindwa kumsajili Mzambia mwingine, Winston Kalengo.
Yanga ilikuwa na mpango wa kumsajili Kalengo
kutokea Zesco ya nyumbani kwao ili kuchukua nafasi ya Chirwa ambaye walitaka
kumpeleka kwa mkopo katika timu yake ya zamani ya FC Platinum.
Mpaka usiku wa kuamkia jana ambapo usajili wa
dirisha dogo ulifungwa, Yanga ilikuwa na mpango huo, lakini kikao kizito
walichokaa na mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji, kiliamua waachane naye na
kubaki na Chirwa ambaye kwa mwezi anachukua dola 2,500 ambazo ni sawa zaidi ya
Sh milioni 5.
Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kimesema: “Kalengo
alikuwa anataka alipwe mshahara mkubwa kuliko huu wa Chirwa, hicho ndicho
kilikuwa kikwazo kikubwa kwani ilikuwa haiwezekani Kalengo alipwe pesa hiyo,
halafu Chirwa naye alipwe na Yanga akiwa kule Platinum ambako alitakiwa
kupelekwa kwa mkopo.
“Awali kocha mkuu hakutaka kumuachia Chirwa
lakini kuna baadhi ya watu ndiyo walitaka dili hilo lifanyike, mwenyekiti
akasema asikilizwe kocha matakwa yake na siyo kumuingilia, hapo ndipo dili la
Kalengo likafa kabisa, chanzo kikubwa ni huo mshahara lakini pia ishu ya kocha
kuridhika na wachezaji alionao.”
Mpaka usajili wa dirisha dogo unafungwa juzi,
Yanga imewasajili Mzambia, Justine Zulu aliyekuwa akiichezea Zesco ya nyumbani
kwao na Emmanuel Martin aliyetokea JKU ya Zanzibar, huku ikiachana na
Mnyarwanda, Mbuyu Twite aliyemaliza mkataba.
Post a Comment