KAMATI ya Usajili ya Simba
chini ya mwenyekiti wake Zakaria Hans Poppe, imesema kuwa kwenye usajili wao wa
dirisha dogo la usajili, ni lazima wamsajili beki mwingine mwenye uwezo kama
Mganda, Juuko Murshid.
Dirisha dogo la usajili
tayari limefunguliwa tangu Novemba 15 na litafungwa Desemba 15, mwaka huu kwa
timu zote shiriki za Ligi Kuu Bara.
Nafasi hiyo ya beki wa kati
inayochezwa na Juuko, huwa inachezwa pia na Emmanuel Semwanza na Novalty
Lufunga.
Akizungumza na Championi
Jumatatu, Hans Poppe alisema watamsajili beki wa kati mwingine, kwa kuwa
watamkosa Juuko kwa miezi miwili kutokana na kutakiwa kwenda kushiriki michuano
ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) inayotarajiwa kufanyika Januari, mwakani.
Hans Poppe alisema, beki
huyo wanayemhitaji ni yule atakayeweza kupambana na washambuliaji wasumbufu.
“Tunatarajia kumkosa Juuko
kwa kipindi cha miezi miwili atakachokuwepo na majukumu ya timu yake ya taifa
ya Uganda itakayokuwa inashiriki michuano ya Afcon.
“Hivyo, anatarajia kuzikosa
baadhi ya mechi za mwanzoni za mzunguko wa pili wa ligi kuu, hivyo ni lazima
tumtafute beki mwingine mwenye sifa kama zake za kupambana na washambuliaji
wasumbufu.
“Kama kamati husika, hivi
sasa tupo kwenye michakato ya kumsajili beki huyo tunayemhitaji atakayecheza
pamoja na beki wetu, Mwanjale (Method) katika kipindi ambacho Juuko hayupo,”
alisema Hans Poppe.
Post a Comment