STRAIKA mpya wa Yanga, Emmanuel Martin, ameweka wazi
kuwa anafurahia kupewa jezi iliyokuwa ikivaliwa na kiungo wa zamani wa timu
hiyo, Frank Domayo ‘Chumvi’.
Martin aliyejiunga na Yanga hivi karibuni akitokea JKU
ya Zanzibar, ameanza kuvaa jezi namba 18 juzi Alhamisi alipoanza rasmi mazoezi
na kikosi hicho baada ya kuingia kandarasi ya miaka miwili ya kuitumikia timu
hiyo. Jezi hiyo haikuwa imetumika kwa muda mrefu tangu Domayo aondoke Yanga
mwaka 2014.
Martin alisema kwamba, amepata faraja kubwa baada ya
kugundua kuwa jezi hiyo ilikuwa ikivaliwa na kipenzi cha Wanayanga, lakini leo
imekuwa yake, hivyo ni jambo la heri sana kwake.
“Wakati naenda kukabidhiwa jezi, chaguo langu lilikuwa
ni namba 19, ambayo nilikuwa nikivaa JKU, hivyo kwa bahati mbaya hapa nimekuta
anaivaa Geoffrey Mwashiuya, hivyo sikuwa na namna kwani tayari zilikuwa
zimebaki jezi mbili tu ambazo ni namba 18 na 2.
“Kutokana na hilo niliomba hiyo 18, lakini baadaye
nilifurahi sana baada ya kugundua jezi hiyo ilikuwa ikivaliwa na Domayo, ambaye
alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga, hivyo ni jambo la faraja kwangu,”
alisema Martin.
Post a Comment