Simba ikicheza vyema karata hizi, ubingwa wao 2016/17
WAKATI Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikitarajia kuanza Jumamosi, Simba wataanza kuusaka ubingwa Dar es Salaam, ambao wana mechi saba za mzunguko wa kwanza katika uwanja wao wa nyumbani wa Taifa.
Simba wakifanikiwa kushinda mechi hizo watakuwa wamejisafishia njia ya kutwaa ubingwa wa msimu mpya, kwani watakuwa wamefikisha pointi 21 kabla ya kutoka nje ya Jiji la Dar es Salaam kucheza mechi za ugenini.
Katika mchezo wao wa kwanza wanatarajia kucheza na Ndanda utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, kabla ya kukutana na JKT Ruvu Agosti 27, mwaka huu.
Simba ambao hawajaonja ubingwa kwa misimu minne, watacheza mechi ya nne dhidi ya Mtibwa Sugar, Septemba 11, kabla ya kucheza na Azam Septemba 17, kisha Majimaji Septemba 24 na baadaye kuwavaa mahasimu wao wa jadi, Yanga Oktoba mosi mwaka huu.
Akizungumza na BINGWA jana Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema mikakati yao ni kuhakikisha wanashinda mechi zote ili kujiweka katika mazingira bora ya kuchukua ubingwa wa ligi hiyo.
Manara alisema kamati ya utendaji ya klabu hiyo leo itafanya mazungumzo maalumu na wachezaji sambamba na benchi la ufundi kwa lengo la kupanga mikakati ya ushindi dhidi ya Ndanda.
“Tunajua umuhimu wa mechi yetu na Ndanda, benchi la ufundi litakutana kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji ili kuhakikisha tunashinda kwenye mchezo huo,” alisema.
Alisema msimu huu wamedhamiria kurudisha heshima baada ya kushindwa kutamba kwa miaka minne na kuwaacha wapinzani wao Yanga na Azam wakipokezana kwa zamu kushiriki michuano ya kimataifa.
Post a Comment