MAMBO safii! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba kufikia uamuzi wa kukubali uwekezaji wa mfanyabiashara, Mohamed Dewji ‘Mo’, katika klabu hiyo.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao cha pamoja na Mo kilichofanyika juzi Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Simba iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara,  kikao  hicho kilikuwa ni mwendelezo wa Mkutano Mkuu wa wanachama wa Julai 31 mwaka huu, ulioridhia kuwepo kwa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu yao.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Mo aliwaeleza wajumbe wa kamati ya utendaji dhamira yake ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh bilioni 20, lakini akitoa ahadi ya kuwawezesha wanachama wa muda mrefu kupewa hisa bure ambazo wataamua wenyewe kuuza au kununua hisa zaidi.
Ilisema kamati imefikia uamuzi wa kukubali uendeshaji wa mfumo mpya wa klabu hiyo kutokana na kutambua  kwamba wanahitaji  fedha nyingi ili klabu iweze kushindana na klabu nyingine kubwa barani Afrika, hivyo ni sahihi kuhamia katika mfumo wa hisa.
“Kimsingi fedha nyingi zinahitajika kuendesha klabu kama Simba ili iwe na uwezo wa kununua wachezaji wazuri, viwanja, majengo na hatimaye ubavu wa kushindana na timu nyingine kubwa Afrika na si Tanzania pekee, kutokana na Mo kueleza nia yake na anafanya hayo kutokana na mapenzi yake na klabu,  hivyo tumekubaliana na ombi alilolileta kwetu.
“Anataka kuitoa klabu kwenye bajeti ya bilioni 1.2 kwa mwaka hadi bilioni 5.5 na kwa kuamini mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio, lakini  ameahidi kufanya usajili mzuri, kocha mwenye viwango, mambo yote yanaweza kugharimu Sh bilioni nne na kwamba Sh bilioni 1.5 itakayobaki, ataiweka katika mradi wa ujenzi wa uwanja,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema mchakato wa kuingia katika mabadiliko ya mfumo utachukua miezi sita mpaka kukamilika kuanzia kipindi hiki cha mpito na wanachama wa Simba wataendelea kupatiwa elimu kuhusu mfumo mpya ili kila atakayenunua hisa atambue haki na wajibu wake.
Kutokana na hali hiyo, mpango huo utakamilika Januari ambapo Simba itaanza kufaidi matunda ya Mo ambaye aliwahi kuwa mfadhali wa klabu hiyo  kati ya 1999 na 2005 na kuweza kuyashawishi makampuni ya Simba Cement na NBC kuwekeza na baadaye kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 kwa kuitoa Zamalek ya Misri.
Mbali na Simba, Mo amewahi pia kuwa mdhamini wa Singida United na mmiliki wa African Lyon kwa muda, kabla ya kuiuza kwa mfanyabiashara Rahim ‘Zamunda’ Kangenzi.

Post a Comment

 
Top